Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 10:1-22

Ezekieli 10:1-22 NEN

Nikatazama, nikaona juu ya ile nafasi iliyokuwa juu ya vichwa vya wale makerubi kulikuwa na kitu mfano wa kiti cha enzi cha yakuti samawi. BWANA akamwambia mtu yule aliyekuwa amevaa nguo ya kitani, “Ingia katikati ya yale Magurudumu yaliyo chini ya makerubi. Ukaijaze mikono yako makaa ya mawe ya moto kutoka katikati ya makerubi na uyatawanye juu ya mji.” Nilipokuwa nikiangalia, akaingia ndani. Basi wale makerubi walikuwa wamesimama upande wa kusini wa Hekalu wakati yule mtu alipoingia ndani, wingu likaujaza ule ukumbi wa ndani. Kisha utukufu wa BWANA ukainuka kutoka juu ya wale makerubi ukaenda kwenye kizingiti cha Hekalu. Wingu likajaza Hekalu, nao ukumbi ukajawa na mngʼao wa utukufu wa BWANA. Sauti ya mabawa ya wale makerubi ingeweza kusikika mpaka kwenye ukumbi wa nje, kama sauti ya Mungu Mwenyezi wakati anapoongea. BWANA alipomwamuru yule mtu aliyevaa nguo za kitani akisema, “Chukua moto toka katikati ya magurudumu, kutoka katikati ya makerubi,” yule mtu aliingia ndani akasimama pembeni mwa gurudumu. Ndipo mmoja wa wale makerubi akanyoosha mkono wake kwenye moto uliokuwa katikati yao. Akachukua baadhi ya moto na kuutia mikononi mwa yule mtu aliyevaa mavazi ya kitani, naye akaupokea akatoka nje. (Chini ya mabawa ya makerubi paliweza kuonekana kitu kilichofanana na mikono ya mwanadamu.) Nikatazama, nikaona magurudumu manne kando ya makerubi, moja kando ya kila kerubi. Magurudumu hayo yalimetameta kama kito cha zabarajadi. Kule kuonekana kwake, yote manne yalifanana kila gurudumu lilikuwa kama linazunguka ndani ya lingine. Yalipozunguka, yalikwenda kokote katika pande nne walikoelekea wale makerubi. Magurudumu hayakugeuka wakati makerubi yalipokwenda. Makerubi walikwenda upande wowote kichwa kilikoelekea pasipo kugeuka walipokuwa wakienda. Miili yao yote, pamoja na migongo yao, mikono na mabawa yao yote yalikuwa yamejaa macho kabisa kama yalivyokuwa yale magurudumu yao manne. Nikasikia magurudumu yakiitwa, “Magurudumu ya kisulisuli.” Kila mmoja wa wale makerubi alikuwa na nyuso nne: Uso mmoja ulikuwa kama vile wa kerubi, uso wa pili ulikuwa wa mwanadamu, uso wa tatu ulikuwa wa simba na uso wa nne ulikuwa wa tai. Kisha makerubi wakapaa juu. Hawa ndio wale viumbe walio hai niliowaona kando ya Mto Kebari. Wakati makerubi walipokwenda, magurudumu yaliyoko kando yao yalikwenda na wakati makerubi walipotanda mabawa yao wapate kupaa juu kutoka ardhi, magurudumu yale hayakuondoka pembeni mwao. Makerubi yaliposimama kimya, nayo pia yalitulia kimya, nao makerubi yalipoinuka juu, magurudumu nayo yaliinuka juu pamoja nao, kwa sababu roho ya vile viumbe hai ilikuwa ndani yake. Kisha utukufu wa BWANA ukaondoka pale kwenye kizingiti cha Hekalu na kusimama juu ya wale makerubi. Nilipokuwa nikitazama, makerubi yakatanda mabawa yao na kuinuka kutoka ardhini, nao walipokuwa wakienda, yale magurudumu yakaenda pamoja nao. Wakasimama kwenye ingilio la lango la mashariki la nyumba ya BWANA, nao utukufu wa Mungu wa Israeli ukawa juu yao. Hawa walikuwa ndio viumbe hai niliokuwa nimewaona chini ya Mungu wa Israeli kando ya Mto Kebari, nami nikatambua ya kuwa hao walikuwa makerubi. Kila mmoja alikuwa na nyuso nne, mabawa manne, chini ya mabawa yao kulikuwa na kile kilichoonekana kama mikono ya mwanadamu. Nyuso zao zilifanana kama zile nilizokuwa nimeziona kando ya Mto Kebari. Kila mmoja alikwenda mbele moja kwa moja.