Ezekieli 1:15-28
Ezekieli 1:15-28 NENO
Nilipokuwa nikitazama wale viumbe hai, niliona gurudumu moja juu ya ardhi kando ya kila kiumbe na nyuso zake nne. Hivi ndivyo ilivyokuwa kuonekana kwa hayo magurudumu na muundo wake: yalimetameta kama zabarajadi, nayo yote manne yalifanana. Kila gurudumu lilionekana kuwa na gurudumu lingine ndani yake. Magurudumu yalipoenda, yalielekea upande mmoja wa pande nne walikoelekea wale viumbe; wale viumbe walipoenda, magurudumu hayakugeuka. Kingo za magurudumu zilikuwa ndefu kwenda juu na za kutisha, nazo zote nne zilijawa na macho pande zote. Wale viumbe hai walipoenda, magurudumu yaliyokuwa kando yao yalisogea; wakati hao viumbe hai walipoinuka kutoka ardhini, magurudumu nayo yaliinuka. Popote roho alipoenda, wale viumbe nao walienda, nayo magurudumu yaliinuka pamoja nao, kwa sababu roho ya wale viumbe hai alikuwa ndani ya hayo magurudumu. Viumbe wale waliposogea, nayo magurudumu yalisogea; viumbe waliposimama, nayo pia yalisimama; viumbe walipoinuka juu ya nchi, magurudumu yaliinuka pamoja nao, kwa kuwa roho ya hao viumbe hai alikuwa ndani ya hayo magurudumu. Juu ya vichwa vya hao viumbe hai palikuwa na kitu mfano wa eneo lililokuwa wazi, lililokuwa angavu kabisa na la kutisha. Chini ya hiyo nafasi, mabawa yao yalitanda moja kuelekea lingine, na kila mmoja alikuwa na mabawa mawili yaliyofunika mwili wake. Viumbe wale waliposogea, nilisikia sauti ya mabawa yao, kama ngurumo ya maji yaendayo kasi, kama sauti ya Mwenyezi, kama kishindo cha jeshi. Waliposimama, walishusha mabawa yao. Ndipo ikaja sauti toka juu ya ile nafasi ya wazi iliyokuwa juu ya vichwa vyao, waliposimama mabawa yao yakiwa yameshushwa. Juu ya ile nafasi ya wazi iliyokuwa juu ya vichwa vyao, kulikuwa na kitu mfano wa kiti cha utawala cha yakuti samawi. Na juu ya kile kiti cha utawala kulikuwa na umbo, mfano wa mwanadamu. Nikaona kwamba kutokana na kile kilichoonekana kuwa kiuno chake kuelekea juu, alionekana kama chuma inavyong’aa ikiwa ndani ya moto, na kuanzia kiuno kwenda chini alionekana kama moto; mwanga wenye kung’aa sana ulimzunguka. Kama vile kuonekana kwa upinde wa mvua mawinguni siku ya mvua, ndivyo ulivyokuwa ule mng’ao uliomzunguka. Hivi ndivyo mfano wa utukufu wa Mwenyezi Mungu ulionekana. Nilipouona, nikaanguka kifudifudi, nikasikia sauti ya mtu anaongea.