Kutoka 6:1-8
Kutoka 6:1-8 NEN
Kisha BWANA akamwambia Mose, “Sasa utaona kitu nitakachomfanyia Farao: Kwa sababu ya mkono wangu wenye nguvu atawaachia watu waende; kwa sababu ya mkono wangu wenye nguvu atawafukuza waondoke nchini mwake.” Pia Mungu akamwambia Mose, “Mimi ndimi BWANA. Nilimtokea Abrahamu, Isaki na Yakobo kama Mungu Mwenyezi, ingawa sikuwajulisha Jina langu, Yehova, Mimi mwenyewe sikujitambulisha kwao. Pia niliweka Agano langu nao kuwapa nchi ya Kanaani, ambako waliishi kama wageni. Zaidi ya hayo, nimesikia kilio cha huzuni cha Waisraeli ambao Wamisri wamewatia utumwani, nami nimelikumbuka Agano langu. “Kwa hiyo, waambie Waisraeli: ‘Mimi ndimi BWANA, nami nitawatoa mtoke katika kongwa la Wamisri. Nitawaweka huru mtoke kuwa watumwa wao, nami nitawakomboa kwa mkono ulionyooshwa pamoja na matendo makuu ya hukumu. Nitawatwaa mwe watu wangu mwenyewe, nami nitakuwa Mungu wenu. Ndipo mtajua kuwa mimi ndimi BWANA Mungu wenu, niliyewatoa chini ya kongwa la Wamisri. Nami nitawaleta mpaka nchi niliyoapa kwa mkono ulioinuliwa kumpa Abrahamu, Isaki na Yakobo. Nitawapa iwe milki yenu. Mimi ndimi BWANA.’ ”