Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kutoka 4

4
Ishara za Musa
1Musa akamjibu, “Itakuwaje wasiponiamini au kunisikiliza, waseme, ‘Mwenyezi Mungu hakukutokea’?”
2Ndipo Mwenyezi Mungu akamuuliza, “Ni nini hicho kilicho mkononi mwako?”
Akamjibu, “Ni fimbo.”
3Mwenyezi Mungu akasema, “Itupe chini.”
Musa akaitupa fimbo chini, nayo ikawa nyoka, naye akaikimbia. 4Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia, “Nyoosha mkono wako umkamate kwenye mkia.” Basi Musa akanyoosha mkono akamkamata yule nyoka, naye akabadilika tena kuwa fimbo mkononi mwake. 5Mwenyezi Mungu akasema, “Hivi ndivyo Waisraeli watakavyoamini kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zao, Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo, amekutokea wewe.”
6Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia, “Weka mkono wako ndani ya joho lako.” Basi Musa akaweka mkono wake ndani ya joho lake, naye alipoutoa, ulikuwa na ukoma, mweupe kama theluji.
7Mungu akamwambia, “Sasa urudishe tena huo mkono ndani ya joho lako.” Basi Musa akaurudisha mkono wake ndani ya joho lake na alipoutoa, ulikuwa mzima, kama sehemu zingine za mwili wake.
8Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia, “Kama hawatakuamini wewe, au kutojali ishara ya kwanza, wataamini ishara ya pili. 9Lakini kama hawataamini ishara hizi mbili au hawatawasikiliza ninyi, chukua kiasi cha maji kutoka Mto Naili uyamimine juu ya ardhi kavu. Maji mtakayotoa mtoni yatakuwa damu juu ya ardhi.”
10Musa akamwambia Mwenyezi Mungu, “Ee Bwana, kamwe sijapata kuwa msemaji kwa ufasaha hapo awali, wala tangu ulipoanza kuzungumza na mtumishi wako. Ulimi wangu ni mzito kuzungumza.”
11Mwenyezi Mungu akamwambia, “Ni nani aliyempa mwanadamu kinywa? Ni nani aliyemfanya mtu kuwa kiziwi au bubu? Ni nani anayempa mtu uwezo wa kuona au upofu? Je, si mimi, Mwenyezi Mungu? 12Sasa nenda, nitakusaidia kusema, nami nitakufundisha jambo la kusema.”
13Lakini Musa akasema, “Ee Bwana, tafadhali mtume mtu mwingine kufanya kazi hiyo.”
14Ndipo hasira ya Mwenyezi Mungu ikawaka dhidi ya Musa, akamwambia, “Vipi kuhusu ndugu yako, Haruni Mlawi? Ninajua yeye anaweza kuzungumza vizuri. Naye yuko tayari njiani kukulaki, na moyo wake utafurahi wakati atakapokuona. 15Utazungumza naye na kuweka maneno kinywani mwake. Nitawasaidia ninyi wawili kusema, nami nitawafundisha jambo la kufanya. 16Haruni ataongea na watu badala yako na itakuwa kwamba yeye amekuwa kinywa chako nawe utakuwa kama Mungu kwake. 17Lakini chukua fimbo hii mkononi mwako ili uweze kuitumia kufanya ishara hizo za ajabu.”
Musa anarudi Misri
18Kisha Musa akarudi kwa Yethro mkwewe akamwambia, “Niruhusu nirudi kwa watu wangu Misri kuona kama yuko hata mmoja wao ambaye bado anaishi.”
Yethro akamwambia, “Nenda, nami nakutakia mema.”
19Basi Mwenyezi Mungu alikuwa amemwambia Musa huko Midiani, “Rudi Misri kwa maana watu wote waliotaka kukuua wamekufa.” 20Basi Musa akamchukua mkewe na wanawe, akawapandisha juu ya punda na kuanza safari kurudi Misri. Naye akaichukua ile fimbo ya Mungu mkononi mwake.
21Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Utakaporudi Misri, hakikisha kwamba utafanya mbele ya Farao maajabu yote niliyokupa uwezo wa kuyafanya. Lakini nitafanya moyo wake kuwa mgumu ili asiwaruhusu watu waende. 22Kisha mwambie Farao, ‘Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: Israeli ni mwanangu mzaliwa wa kwanza, 23nami nilikuambia, “Ruhusu mwanangu aondoke, ili aweze kuniabudu mimi.” Lakini ukakataa kumruhusu aende; basi nitaua mwana wako mzaliwa wa kwanza.’ ”
24Musa alipokuwa mahali pa kulala wageni akiwa njiani kurudi Misri, Mwenyezi Mungu akakutana naye, akataka kumuua. 25Lakini Sipora akachukua kisu cha gumegume, akakata govi la mwanawe na kugusa miguu ya Musa nalo. Sipora akasema, “Hakika wewe ni bwana arusi wa damu kwangu.” 26(Sipora alipomwita Musa, “Bwana arusi wa damu”, alikuwa anamaanisha ile tohara.) Baada ya hayo Mwenyezi Mungu akamwacha.
27Mwenyezi Mungu akamwambia Haruni, “Nenda jangwani ukamlaki Musa.” Basi akakutana na Musa kwenye mlima wa Mungu, akambusu. 28Kisha Musa akamwambia Haruni kila kitu Mwenyezi Mungu alichomtuma kusema, vilevile habari za ishara na maajabu alizokuwa amemwamuru kufanya.
29Musa na Haruni wakawakusanya wazee wote wa Waisraeli, 30naye Haruni akawaambia kila kitu Mwenyezi Mungu alichokuwa amemwambia Musa. Pia akafanya ishara mbele ya watu, 31nao wakaamini. Nao waliposikia kuwa Mwenyezi Mungu anajishughulisha nao, na kwamba ameona mateso yao, walisujudu na kuabudu.

Iliyochaguliwa sasa

Kutoka 4: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia