Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kutoka 38:21-31

Kutoka 38:21-31 NEN

Ifuatayo ni orodha ya vifaa vilivyotumika kwa ajili ya ujenzi wa maskani, maskani ya Ushuhuda, ambavyo vilitayarishwa na Walawi kama alivyoagiza Mose, chini ya usimamizi wa Ithamari, mwana wa kuhani Aroni. (Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa kabila la Yuda, alifanya kila kitu BWANA alichomwamuru Mose, akiwa pamoja na Oholiabu mwana wa Ahisamaki, wa kabila la Dani, fundi stadi wa kutia nakshi, kubuni michoro, mtarizi kwa rangi ya buluu, ya zambarau, nyekundu na kitani safi.) Jumla ya dhahabu iliyopatikana kutokana na sadaka ya kuinuliwa kwa ajili ya kazi ya mahali patakatifu ilikuwa na uzito wa talanta 29 na shekeli 730, kulingana na shekeli ya mahali patakatifu. Fedha iliyopatikana kutokana na jumuiya ya watu waliohesabiwa ilikuwa yenye uzito wa talanta mia moja na shekeli 1,775, kulingana na shekeli ya mahali patakatifu. Kila mtu alitoa beka moja, ambayo ni sawa na nusu shekeli ya fedha, kwa kazi ya mahali patakatifu, kutoka kwa kila mtu aliyekuwa amehesabiwa mwenye umri wa miaka ishirini au zaidi, ambao jumla yao walikuwa wanaume 603,550. Talanta hizo 100 za fedha zilitumika kusubu vile vitako mia moja kwa ajili ya mahali patakatifu na pazia: vitako mia moja kwa talanta mia, yaani, talanta moja kwa kila kitako. Akatumia zile shekeli hizo 1,775 kutengeneza kulabu za nguzo, kufunika ncha za nguzo na kutengeneza vitanzi vyake. Shaba iliyopatikana kutokana na sadaka ya kuinuliwa ilikuwa na uzito wa talanta 70 na shekeli 2,400. Akaitumia hiyo shaba kutengeneza vitako vya ingilio la Hema la Kukutania, madhabahu ya shaba pamoja na ule wavu wake na vyombo vyake vyote, vile vitako vya ule ua uliozunguka na vile vya ingilio, na vigingi vyote vya Maskani pamoja na ule ua uliozunguka.