Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kutoka 32:7-18

Kutoka 32:7-18 NEN

Kisha BWANA akamwambia Mose, “Shuka, kwa sababu watu wako, uliowatoa Misri, wamepotoka. Wamekuwa wepesi kugeuka na kuacha niliyowaamuru, na wamejitengenezea sanamu ya kuyeyusha yenye umbo la ndama. Wameisujudia na kuitolea dhabihu, nao wamesema, ‘Hii ndiyo miungu yenu, ee Israeli iliyokupandisha kutoka Misri.’ ” BWANA akamwambia Mose, “Nimeona watu hawa, nao ni watu wenye shingo ngumu. Sasa niache ili hasira yangu ipate kuwaka dhidi yao, nami nipate kuwaangamiza. Kisha nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa.” Lakini Mose akamsihi BWANA Mungu wake, akasema, “Ee BWANA, kwa nini hasira yako iwake dhidi ya watu wako, wale uliowatoa Misri kwa uweza mkuu na mkono wenye nguvu? Kwa nini Wamisri waseme, ‘Ni kwa nia mbaya aliwatoa Misri, ili awaue milimani na kuwafuta usoni mwa dunia’? Achilia mbali hasira yako kali, waonee huruma na usilete maafa juu ya watu wako. Wakumbuke watumishi wako Abrahamu, Isaki na Israeli, ambao uliwaapia kwa nafsi yako mwenyewe: ‘Nitawafanya uzao wako kuwa wengi kama nyota za angani, nami nitawapa wazao wako nchi hii yote ambayo niliwaahidia, nayo itakuwa urithi wao milele.’ ” Kisha BWANA akawaonea huruma, wala hakuleta juu ya watu wake maafa aliyokuwa amekusudia. Mose akageuka, akashuka kutoka mlimani akiwa na vibao viwili vya Ushuhuda mikononi mwake. Vilikuwa vimeandikwa pande zote mbili, mbele na nyuma. Vibao hivyo vilikuwa kazi ya Mungu; maandishi yalikuwa mwandiko wa Mungu, yaliyochorwa kama muhuri juu ya vibao. Yoshua aliposikia sauti za watu wakipiga kelele, akamwambia Mose, “Kuna sauti ya vita kambini.” Mose akajibu: “Si sauti ya ushindi, wala si sauti ya kushindwa; ni sauti ya kuimba ninayosikia.”

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Kutoka 32:7-18