Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kutoka 25

25
Sadaka Kwa Ajili Ya Maskani Ya Mungu
(Kutoka 35:4-9)
1 Bwana akamwambia Mose, 2“Waambie Waisraeli waniletee sadaka. Utapokea sadaka kwa niaba yangu kutoka kwa kila mtu ambaye moyo wake wapenda kutoa. 3Hizi ndizo sadaka utakazozipokea kutoka kwao: dhahabu, fedha na shaba; 4 nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, za rangi nyekundu, pamoja na kitani safi; singa za mbuzi; 5 ngozi za kondoo dume zilizopakwa rangi nyekundu, na ngozi za pomboo;#25:5 Pomboo hapa ina maana ya mnyama mwenye ngozi laini aishiye kwenye milima yenye misitu, au pengine nguva au sili. mbao za mshita; 6 mafuta ya zeituni kwa ajili ya taa; vikolezi kwa ajili ya mafuta ya upako, pamoja na uvumba wa harufu nzuri; 7 na vito vya shohamu na vito vingine vya thamani vya kuweka kwenye kisibau na kile kifuko cha kifuani.
8 “Kisha uwaamuru wanitengenezee mahali patakatifu, nami nitakaa miongoni mwao. 9 Tengeneza hema hili na vyombo vyake vyote sawasawa na kielelezo nitakachokuonyesha.
Sanduku La Agano
(Kutoka 37:1-9)
10 “Nao watatengeneza Sanduku la mbao za mshita, lenye urefu wa dhiraa mbili na nusu,#25:10 Dhiraa mbili na nusu ni sawa na sentimita 112.5. upana wa dhiraa moja na nusu,#25:10 Dhiraa moja na nusu ni sawa na sentimita 67.5. na kimo cha dhiraa moja na nusu. 11 Utalifunika hilo Sanduku kwa dhahabu safi ndani na nje, na kulifanyia ukingo wa dhahabu juu yake kulizunguka. 12Utalisubu kwa pete nne za dhahabu na kuzifungia kwenye miguu yake minne, pete mbili kwa upande mmoja na pete mbili kwa upande mwingine. 13 Kisha utatengeneza mipiko ya mti wa mshita na kuzifunika kwa dhahabu. 14 Utaiingiza hiyo mipiko kwenye zile pete katika pande mbili za Sanduku ili kulibeba. 15 Hiyo mipiko itabakia daima katika hizo pete za hilo Sanduku; haitaondolewa. 16 Kisha weka ndani ya hilo Sanduku ule Ushuhuda nitakaokupa.
17 “Tengeneza kifuniko cha upatanisho cha dhahabu safi, chenye urefu wa dhiraa mbili na nusu, na upana wa dhiraa moja na nusu. 18 Tengeneza makerubi wawili wa dhahabu iliyofuliwa katika miisho ya hicho kifuniko. 19Tengeneza kerubi mmoja kwenye mwisho mmoja, na kerubi mwingine kwenye mwisho mwingine; watengeneze makerubi hao wawe kitu kimoja na hicho kifuniko katika miisho hiyo miwili. 20 Makerubi hao watakuwa wametandaza mabawa kuelekea juu, yakitia kivuli hicho kifuniko. Makerubi hao wataelekeana, wakitazama hicho kifuniko. 21 Weka huo Ushuhuda nitakaokupa ndani ya hilo Sanduku la Agano, na uweke hicho kifuniko juu ya hilo Sanduku. 22 Hapo juu ya hicho kifuniko, kati ya hao makerubi wawili walioko juu ya hilo Sanduku la Ushuhuda, hapo ndipo nitakapokutana nawe na kukupa maagizo yangu kwa ajili ya Waisraeli.
Meza Ya Mikate Ya Wonyesho
(Kutoka 37:10-16)
23 “Tengeneza meza ya mbao za mshita yenye urefu wa dhiraa mbili,#25:23 Dhiraa mbili ni sawa na sentimita 90. upana wa dhiraa moja, na kimo cha dhiraa moja na nusu. 24Ifunike kwa dhahabu safi, na kuitengenezea ukingo wa dhahabu kuizunguka pande zote. 25Kisha tengeneza upapi wenye upana wa nyanda nne,#25:25 Nyanda nne ni sawa na sentimita 8. na ufanyie ule upapi ukingo wa dhahabu kuuzunguka pande zote. 26Tengeneza pete nne za dhahabu kwa ajili ya meza hiyo, na uzifungie kwenye pembe nne, pale penye miguu yake minne. 27Pete hizo zitakuwa karibu na ukingo ule ili kuishikilia ile mipiko itakayotumika kuibebea hiyo meza. 28Tengeneza mipiko hiyo kwa mbao za mshita, uifunike na dhahabu, uitumie kubeba hiyo meza. 29 Tengeneza sahani zake na masinia yake kwa dhahabu safi, pamoja na bilauri na bakuli zake kwa ajili ya kumiminia sadaka. 30 Utaweka mikate ya Wonyesho juu ya meza hii iwe mbele yangu daima.
Kinara Cha Taa
(Kutoka 37:17-24)
31 “Tengeneza kinara cha taa cha dhahabu safi iliyofuliwa vizuri katika kitako chake na ufito wake; vikombe vyake vinavyofanana na ua, matovu yake na maua yake viwe kitu kimoja. 32 Matawi sita yatatokeza kuanzia ule ufito wa katikati wa kinara cha taa: matawi matatu upande mmoja na matatu upande mwingine. 33Vikombe vitatu vya mfano wa maua ya mlozi yenye matovu na maua vitakuwa katika tawi moja, vikombe vitatu katika tawi jingine, na vivyo hivyo kwa matawi yote sita yanayotokeza kwenye kile kinara cha taa. 34Juu ya kinara chenyewe vitakuwepo vikombe vinne vya mfano wa maua ya mlozi yakiwa na matovu yake na maua yake. 35Tovu moja litakuwa chini ya jozi ya kwanza ya matawi yaliyotokeza kwenye kinara cha taa, tovu la pili chini ya jozi ya pili, nalo tovu la tatu chini ya jozi ya tatu, yaani matawi sita kwa jumla. 36 Matovu na matawi yote yatakuwa kitu kimoja na kile kinara cha taa, yakifuliwa kwa dhahabu safi.
37 “Kisha tengeneza taa zake saba na uziweke juu ya kinara hicho ili ziangaze mbele yake. 38 Mikasi ya kusawazishia tambi, pamoja na masinia, zote zitakuwa za dhahabu safi. 39Utatumia talanta moja#25:39 Talanta moja ya dhahabu ni sawa na kilo 34. ya dhahabu safi kutengeneza hicho kinara na vifaa vyake vyote. 40 Hakikisha kuwa umevitengeneza sawasawa na ule mfano ulioonyeshwa kule mlimani.

Iliyochaguliwa sasa

Kutoka 25: NEN

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia