Kutoka 24:1-8
Kutoka 24:1-8 NENO
Kisha Mungu akamwambia Musa, “Njooni huku juu kwa Mwenyezi Mungu, wewe na Haruni, Nadabu na Abihu, pamoja na wazee sabini wa Israeli. Mniabudu kwa mbali, lakini Musa peke yake ndiye atakayemkaribia Mwenyezi Mungu; wengine wasije karibu. Nao watu wasije wakapanda pamoja naye.” Musa alipoenda na kuwaambia watu maneno yote na sheria zote za Mwenyezi Mungu, wakaitikia kwa sauti moja, “Kila kitu alichosema Mwenyezi Mungu tutakifanya.” Ndipo Musa akaandika kila kitu Mwenyezi Mungu alichokuwa amesema. Akaamka kesho yake asubuhi na mapema na kujenga madhabahu chini ya mlima na kusimamisha nguzo kumi na mbili za mawe kuwakilisha makabila kumi na mawili ya Israeli. Kisha akawatuma vijana wanaume Waisraeli, nao wakatoa sadaka za kuteketezwa na dhabihu za mafahali wachanga kuwa sadaka za amani kwa Mwenyezi Mungu. Musa akachukua nusu ya damu ya wale wanyama na kuiweka kwenye mabakuli, na nusu nyingine akainyunyiza juu ya madhabahu. Kisha akachukua kile Kitabu cha Agano na kuwasomea watu. Nao wakajibu, “Tutafanya kila kitu alichosema Mwenyezi Mungu, nasi tutatii.” Ndipo Musa akachukua ile damu, akawanyunyizia wale watu, akasema, “Hii ni damu ya agano ambalo Mwenyezi Mungu amelifanya nanyi kufuatana na maneno haya yote.”