Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kutoka 24:1-11

Kutoka 24:1-11 NEN

Kisha Mungu akamwambia Mose, “Njooni huku juu kwa BWANA, wewe na Aroni, Nadabu na Abihu, pamoja na wazee sabini wa Israeli. Mniabudu kwa mbali, lakini Mose peke yake ndiye atakayemkaribia BWANA; wengine wasije karibu. Nao watu wasije wakapanda pamoja naye.” Mose alipokwenda na kuwaambia watu maneno yote na sheria zote za BWANA, wakaitikia kwa sauti moja, “Kila kitu alichosema BWANA tutakifanya.” Ndipo Mose akaandika kila kitu BWANA alichokuwa amesema. Akaamka kesho yake asubuhi na mapema na kujenga madhabahu chini ya mlima na kusimamisha nguzo kumi na mbili za mawe kuwakilisha makabila kumi na mawili ya Israeli. Kisha akawatuma vijana wanaume wa Kiisraeli, nao wakatoa sadaka za kuteketezwa na dhabihu za mafahali wachanga kuwa sadaka za amani kwa BWANA. Mose akachukua nusu ya damu ya wale wanyama na kuiweka kwenye mabakuli na nusu nyingine akainyunyiza juu ya madhabahu. Kisha akachukua kile Kitabu cha Agano na kuwasomea watu. Nao wakajibu, “Tutafanya kila kitu alichosema BWANA, nasi tutatii.” Ndipo Mose akachukua ile damu, akawanyunyizia wale watu, akasema, “Hii ni damu ya agano ambalo BWANA amelifanya nanyi kufuatana na maneno haya yote.” Mose na Aroni, Nadabu na Abihu, pamoja na wazee sabini wa Israeli wakapanda mlimani, nao wakamwona Mungu wa Israeli. Chini ya miguu yake kulikuwa na kitu kama sakafu ya mawe ya yakuti samawi, iliyo safi kama anga angavu. Lakini Mungu hakuinua mkono wake dhidi ya hawa viongozi wa Waisraeli; walimwona Mungu, nao wakala na kunywa.

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Kutoka 24:1-11