Kutoka 22:1-6
Kutoka 22:1-6 NENO
“Mtu yeyote akiiba maksai au kondoo na kumchinja au kumuuza, ni lazima alipe ng’ombe watano badala ya maksai mmoja na kondoo wanne badala ya kondoo mmoja. “Mwizi akishikwa akivunja nyumba akapigwa hata akafa, aliyemuua hana hatia ya kumwaga damu; lakini jambo hilo likitokea wakati jua limechomoza, huyo mtu atakuwa na hatia ya kumwaga damu. “Mwizi huyo sharti alipe, lakini kama hana kitu, lazima auzwe ili alipe kwa ajili ya wizi wake. “Mnyama aliyeibwa akikutwa hai mkononi mwake, iwe ni maksai au punda au kondoo, lazima alipe mara mbili. “Mtu akichunga mifugo yake katika shamba au shamba la mizabibu, na akawaachia walishe katika shamba la mtu mwingine, ni lazima alipe vitu bora kutoka shamba lake mwenyewe au kutoka shamba lake la mizabibu. “Moto ukiwaka na kuenea kwenye vichaka vya miiba na kuteketeza miganda ya nafaka au nafaka ambayo haijavunwa, au kuteketeza shamba lote, mtu yule aliyewasha moto lazima alipe.