Kutoka 21:12-27
Kutoka 21:12-27 NEN
“Yeyote ampigaye mtu na kumuua ni lazima auawe hakika. Hata hivyo, kama hakumuua kwa makusudi, lakini Mungu akaruhusu itendeke, basi atakimbilia mahali nitakapomchagulia. Lakini kama mtu akipanga na kumuua mwingine kwa makusudi, mwondoe katika madhabahu yangu na kumuua. “Yeyote amshambuliaye baba yake au mama yake ni lazima auawe. “Yeyote amtekaye nyara mwingine akamuuza au akamweka kwake, akikamatwa ni lazima auawe. “Yeyote atakayemlaani baba yake au mama yake ni lazima auawe. “Kama watu wakigombana na mmoja akimpiga mwingine kwa jiwe au kwa ngumi yake na hakufa bali akaugua na kulala kitandani, yule aliyempiga ngumi hatahesabiwa kuwa na hatia kama mwenzake ataamka na kujikongoja kwa fimbo yake, lakini hata hivyo, ni lazima amlipe fidia ya muda wake aliopoteza na awajibike mpaka apone kabisa. “Kama mtu akimpiga mtumwa wake wa kiume au wa kike kwa fimbo na mtumwa huyo akafa papo hapo, ni lazima aadhibiwe lakini ikiwa mtumwa ataamka baada ya siku moja au mbili, hataadhibiwa, kwa sababu yule mtumwa ni mali yake. “Ikiwa watu wawili wanapigana na wakamuumiza mwanamke mjamzito, naye akazaa kabla ya wakati lakini hakuna majeraha makubwa, mhalifu atatozwa mali kiasi cha madai ya mume wa yule mwanamke, na jinsi mahakama itakavyoamua. Lakini kukiwa na jeraha kubwa, ni lazima ulipe uhai kwa uhai, jicho kwa jicho, jino kwa jino, mkono kwa mkono, mguu kwa mguu, kuchomwa moto kwa kuchomwa moto, jeraha kwa jeraha, mchubuko kwa mchubuko. “Ikiwa mtu atampiga mtumwa mwanaume au mwanamke kwenye jicho na kuliharibu, ni lazima amwache huru yule mtumwa kama fidia ya hilo jicho. Kama akimvunja jino mtumwa wa kiume au wa kike, ni lazima amwache huru huyo mtumwa kwa kufidia hilo jino.