Kutoka 16:27-36
Kutoka 16:27-36 NENO
Hata hivyo, baadhi ya watu wakatoka kwenda kukusanya siku ya saba, lakini hawakupata chochote. Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Je, mtaacha kushika maagizo na maelekezo yangu hadi lini? Fahamuni kuwa Mwenyezi Mungu amewapa ninyi Sabato, ndiyo sababu katika siku ya sita amewapa mikate ya siku mbili. Kila mmoja inampasa kukaa pale alipo katika siku ya saba. Hata mmoja haruhusiwi kutoka.” Kwa hiyo watu wakapumzika siku ya saba. Waisraeli wakaita ile mikate mana. Ilikuwa myeupe kama mbegu za mtama, na ladha yake ilikuwa kama mkate mwembamba uliotengenezwa kwa asali. Musa akasema, “Hivi ndivyo alivyoagiza Mwenyezi Mungu: ‘Chukueni pishi ya mana na kuhifadhi kwa ajili ya vizazi vijavyo ili vione mikate niliyowapa mle jangwani nilipowatoa katika nchi ya Misri.’ ” Kwa hiyo Musa akamwambia Haruni, “Chukua gudulia na uweke pishi moja ya mana ndani yake. Kisha uweke mbele za Mwenyezi Mungu ili kihifadhiwe kwa ajili ya vizazi vijavyo.” Kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza Musa, hatimaye Haruni aliiweka ile mana ndani ya Sanduku la Ushuhuda ili aweze kuihifadhi. Waisraeli wakala mana kwa miaka arobaini, mpaka walipofika katika nchi iliyokaliwa na watu; walikula mana hadi walipofika mpakani mwa Kanaani. (Pishi moja ni sehemu ya kumi ya kipimo cha efa.)