Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kutoka 15

15
Wimbo wa Musa na Miriamu
1Ndipo Musa na Waisraeli wakamwimbia Mwenyezi Mungu wimbo huu:
“Nitamwimbia Mwenyezi Mungu,
kwa kuwa ametukuzwa sana.
Farasi na mpanda farasi
amewatosa baharini.
2“Mwenyezi Mungu ni nguvu zangu na wimbo wangu;
amekuwa wokovu wangu.
Yeye ni Mungu wangu, nami nitamsifu,
Mungu wa baba yangu, nami nitamtukuza.
3Mwenyezi Mungu ni shujaa wa vita;
Mwenyezi Mungu ndilo jina lake.
4Magari ya vita ya Farao na jeshi lake
amewatosa baharini.
Maafisa wa Farao walio bora sana
wamezamishwa katika Bahari ya Shamu.
5Maji yenye kina yamewafunika,
wamezama vilindini kama jiwe.
6Mkono wako wa kuume, Ee Mwenyezi Mungu
ulitukuka kwa uweza.
Mkono wako wa kuume, Ee Mwenyezi Mungu,
ukamponda adui.
7“Katika ukuu wa utukufu wako,
ukawaangusha chini wale waliokupinga.
Uliachia hasira yako kali,
ikawateketeza kama kapi.
8Kwa pumzi ya pua yako
maji yalijilundika.
Mawimbi ya maji yakasimama imara kama ukuta,
vilindi vikagandamana ndani ya moyo wa bahari.
9Adui alijivuna,
‘Nitawafuatia, nitawapata.
Nitagawanya nyara;
nitajishibisha kwao.
Nitafuta upanga wangu
na mkono wangu utawaangamiza.’
10Lakini ulipuliza kwa pumzi yako,
bahari ikawafunika.
Wakazama kama risasi
kwenye maji makuu.
11Ni nani miongoni mwa miungu aliye kama wewe, Ee Mwenyezi Mungu?
Ni nani kama Wewe:
uliyetukuka katika utakatifu,
utishaye katika utukufu,
ukitenda maajabu?
12“Uliunyoosha mkono wako wa kuume
na nchi ikawameza.
13Katika upendo wako usiokoma utawaongoza
watu uliowakomboa.
Katika nguvu zako utawaongoza
hadi makao yako matakatifu.
14Mataifa watasikia na kutetemeka,
uchungu utawakamata Wafilisti.
15Wakuu wa Edomu wataogopa,
viongozi wa Moabu watatetemeka kwa hofu,
Wakanaani watayeyuka,
16vitisho na hofu vitawaangukia.
Kwa nguvu ya mkono wako
watatulia kama jiwe,
hadi watu wako wapite, Ee Mwenyezi Mungu,
hadi watu uliowanunua wapite.
17Utawaingiza na kuwapandikiza
juu ya mlima wa urithi wako:
hapo mahali, Ee Mwenyezi Mungu,
ulipopafanya kuwa makao yako,
mahali patakatifu, Ee Mwenyezi Mungu,
ulipopajenga kwa mikono yako.
18“Mwenyezi Mungu atatawala
milele na milele.”
19Farasi wa Farao, magari yake ya vita na wapanda farasi wake walipoingia baharini, Mwenyezi Mungu aliyarudisha maji ya bahari yakawafunika, lakini Waisraeli walipita baharini mahali pakavu. 20Kisha Miriamu yule nabii mke, ndugu yake Haruni, akachukua matari mkononi mwake na wanawake wote wakamfuata na matari yao wakicheza. 21Miriamu akawaimbia:
“Mwimbieni Mwenyezi Mungu,
kwa maana ametukuka sana.
Farasi na mpanda farasi
amewatosa baharini.”
Maji ya Mara na Elimu
22Kisha Musa akawaongoza Israeli kutoka Bahari ya Shamu na kuingia katika Jangwa la Shuri. Kwa siku tatu walisafiri jangwani bila kupata maji. 23Walipofika Mara, hawakuweza kunywa maji yake kwa sababu yalikuwa machungu. (Ndiyo sababu mahali hapo panaitwa Mara#15:23 maana yake Chungu.) 24Kwa hiyo watu wakamnung’unikia Musa, wakisema, “Tunywe nini?”
25Ndipo Musa akamlilia Mwenyezi Mungu, naye Mwenyezi Mungu akamwonesha kipande cha mti. Akakitupa ndani ya maji, nayo maji yakawa matamu.
Huko Mwenyezi Mungu akawapa amri na sheria na huko akawajaribu. 26Mungu akasema, “Mkisikiliza kwa makini sauti ya Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, na kuyafanya yaliyo mema machoni pake, na mkiyatii maagizo yake na kuzishika amri zake zote, sitaleta juu yenu ugonjwa wowote niliowaletea Wamisri, kwa kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, niwaponyaye.”
27Kisha wakafika Elimu, mahali palipokuwa na chemchemi kumi na mbili, na miti sabini ya mitende, wakapiga kambi huko karibu na maji.

Iliyochaguliwa sasa

Kutoka 15: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia