Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kutoka 14:15-31

Kutoka 14:15-31 NEN

Ndipo BWANA akamwambia Mose, “Kwa nini wewe unanililia? Waambie Waisraeli waendelee mbele. Inua fimbo yako na unyooshe mkono wako juu ya bahari ili kuyagawa maji, hivyo kwamba Waisraeli wapate kupita mahali pakavu baharini. Nitaifanya mioyo ya Wamisri kuwa migumu kusudi waingie baharini wakiwafuatia. Nami nitajipatia utukufu kupitia Farao pamoja na jeshi lake lote, kupitia magari yake ya vita na wapanda farasi wake. Nao Wamisri watajua kwamba Mimi ndimi BWANA nitakapojipatia utukufu kupitia Farao, magari yake ya vita na wapanda farasi wake.” Ndipo malaika wa Mungu, aliyekuwa akisafiri mbele ya jeshi la Israeli, akaondoka akakaa nyuma yao. Pia ile nguzo ya wingu ikaondoka hapo mbele yao na kusimama nyuma, ikakaa kati ya majeshi ya Misri na Israeli. Usiku kucha wingu likaleta giza upande mmoja na nuru kwa upande mwingine, kwa hiyo hakuna aliyemkaribia mwenzake usiku kucha. Ndipo Mose akanyoosha mkono wake juu ya bahari, naye BWANA akayasukuma maji ya bahari nyuma kwa upepo mkali wa mashariki usiku ule wote na kupafanya nchi kavu. Maji yakagawanyika, nao Waisraeli wakapita baharini mahali pakavu, maji yakiwa ukuta upande wao wa kuume na upande wao wa kushoto. Wamisri wakawafuatia ndani ya bahari, pamoja na farasi wote wa Farao, magari ya vita na wapanda farasi. Karibia mapambazuko, BWANA akaliangalia jeshi la Wamisri kutoka ile nguzo ya moto na ya wingu, akalifadhaisha. Mungu akayaondoa magurudumu ya magari yao, kwa hivyo wakayaendesha kwa shida. Nao Wamisri wakasema, “Tuachane na Waisraeli! BWANA anawapigania dhidi ya Misri.” Ndipo BWANA akamwambia Mose, “Nyoosha mkono wako juu ya bahari ili maji yarudiane yawafunike Wamisri, magari yao ya vita na wapanda farasi wao.” Mose akanyoosha mkono wake juu ya bahari, wakati wa mapambazuko bahari ikarudiana na kuwa kama kawaida. Wamisri wakajaribu kuyakimbia maji, lakini BWANA akawasukumia ndani ya bahari. Maji yakarudiana na kuyafunika magari ya vita na wapanda farasi pamoja na jeshi lote la Farao lililokuwa limewafuata Waisraeli ndani ya bahari. Hakuna hata mmoja wao aliyenusurika. Lakini Waisraeli wakapita baharini mahali pakavu, ukiwepo ukuta wa maji upande wao wa kuume na upande wao wa kushoto. Siku ile BWANA akawaokoa Waisraeli kutoka mikononi mwa Wamisri, nao Waisraeli wakawaona Wamisri wamelala ufuoni mwa bahari wakiwa wamekufa. Basi Waisraeli walipoona uwezo mkubwa BWANA aliodhihirisha dhidi ya Wamisri, watu wakamwogopa BWANA na wakaweka tumaini lao kwake na kwa Mose mtumishi wake.

Video for Kutoka 14:15-31

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Kutoka 14:15-31