Kutoka 14:10-18
Kutoka 14:10-18 NENO
Farao alipokaribia, Waisraeli wakainua macho yao, wakawaona Wamisri wakija nyuma yao. Wakashikwa na hofu, wakamlilia BWANA. Wakamwambia Musa, “Je, ni kwamba hakukuwa na makaburi huko Misri hata umetuleta tufe huku jangwani? Umetufanyia nini kututoa Misri? Hatukukuambia tulipokuwa huko Misri, ‘Tuache tuwatumikie Wamisri’? Ingekuwa vyema zaidi kwetu kuwatumikia Wamisri kuliko kufa jangwani!” Musa akawajibu Waisraeli, “Msiogope. Simameni imara, nanyi mtauona wokovu BWANA atakaowapatia leo. Hao Wamisri mnaowaona leo kamwe hamtawaona tena. BWANA atawapigania ninyi, nanyi mnatakiwa kutulia tu.” Ndipo BWANA akamwambia Musa, “Kwa nini wewe unanililia? Waambie Waisraeli waendelee mbele. Inua fimbo yako na unyooshe mkono wako juu ya bahari ili kuyagawa maji, ili Waisraeli wapate kupita mahali pakavu baharini. Nitaifanya mioyo ya Wamisri kuwa migumu kusudi waingie baharini wakiwafuatia. Nami nitajipatia utukufu kupitia Farao pamoja na jeshi lake lote, kupitia magari yake ya vita na wapanda farasi wake. Nao Wamisri watajua kwamba Mimi ndimi BWANA nitakapojipatia utukufu kupitia Farao, magari yake ya vita na wapanda farasi wake.”