Esta 9
9
1Katika siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kumi na mbili, yaani mwezi wa Adari, amri iliyoagizwa na mfalme ilikuwa itekelezwe. Siku hii adui wa Wayahudi walikuwa wametumaini kuwashinda, lakini sasa mambo yaliwageukia na Wayahudi wakawashinda wale waliokuwa wanawachukia. 2Wayahudi walikusanyika katika miji yao, katika majimbo ya Mfalme Ahasuero kuwashambulia wale waliokuwa wanatafuta kuwaangamiza. Hakuna yeyote aliyeweza kushindana nao, kwa sababu watu wa mataifa mengine yote waliwaogopa. 3Nao wakuu wote wa majimbo, majemadari, watawala na maafisa wa mfalme wakawasaidia Wayahudi, kwa sababu walimhofu Mordekai. 4Mordekai alikuwa mtu mashuhuri katika jumba la mfalme; sifa zake zilienea katika majimbo yote naye alipata uwezo zaidi na zaidi.
5Wayahudi waliwaangusha adui zao wote kwa upanga wakiwaua na kuwaangamiza, nao walifanya kile walichotaka kwa wale waliowachukia. 6Katika ngome ya Shushani Wayahudi waliua na kuangamiza wanaume mia tano. 7Pia waliwaua Parshendatha, Dalfoni, Aspatha, 8Poratha, Adalia, Ardatha, 9Parmashta, Arisai, Aridai na Waizatha, 10wana kumi wa Hamani mwana wa Hamedatha, adui wa Wayahudi. Lakini hawakuchukua nyara.
11Mfalme aliarifiwa siku hiyo hiyo hesabu ya waliouawa katika ngome ya Shushani. 12Mfalme akamwambia Malkia Esta, “Wayahudi wamewaua wanaume mia tano, na wana kumi wa Hamani ndani ya ngome ya Shushani. Wamefanyaje katika majimbo mengine ya mfalme yaliyobaki? Je, sasa haja yako ni nini? Nayo pia utapewa. Nalo ombi lako ni nini? Nalo utatendewa.”
13Esta akajibu, “Ikimpendeza mfalme, uwape ruhusa Wayahudi walio Shushani warudie amri ya leo kesho pia, na wana wa Hamani kumi wanyongwe mahali pa kunyongea watu.”
14Basi mfalme akaamuru kwamba hili litendeke. Amri ilitolewa huko Shushani, nao wakawanyonga wana kumi wa Hamani. 15Wayahudi huko Shushani wakakusanyika pamoja siku ya kumi na nne ya mwezi wa Adari, nao wakawaua wanaume mia tatu huko Shushani, lakini hawakuchukua nyara zao.
16Wakati ule ule, Wayahudi wengine waliokuwa kwenye majimbo ya mfalme, wakakusanyika kujilinda nao wakapata nafuu kutokana na adui zao. Waliua adui zao wapatao elfu sabini na tano, lakini hawakugusa nyara zao. 17Hili lilitendeka siku ya kumi na tatu ya mwezi wa Adari na siku ya kumi na nne walipumzika na kuifanya siku ya karamu na furaha.
Kusherehekea Purimu
18Wayahudi huko Shushani, hata hivyo, walikuwa wamekusanyika siku ya kumi na tatu na ya kumi na nne, pia siku ya kumi na tano walipumzika na kuifanya siku ya karamu na furaha.
19Ndiyo sababu Wayahudi wanaokaa vijijini na katika miji midogo huadhimisha siku ya kumi na nne ya mwezi wa Adari kama siku ya furaha na karamu, siku ambayo wao hupeana zawadi mmoja kwa mwingine.
Purimu kuadhimishwa
20Mordekai aliandika matukio haya, naye akapeleka barua kwa Wayahudi wote walio katika majimbo ya Mfalme Ahasuero, majimbo yaliyo mbali na karibu, 21akiwataka kila mwaka washerehekee siku ya kumi na nne na ya kumi na tano ya mwezi wa Adari 22kama wakati ambao Wayahudi walipata nafuu kutoka kwa adui zao na kama mwezi ambao huzuni yao iligeuzwa kuwa furaha na kuomboleza kwao kuwa siku ya kusherehekea. Aliwaandikia kushika siku hizo kama siku za karamu na za furaha na kupeana zawadi za vyakula wao kwa wao na zawadi kwa maskini.
23Hivyo Wayahudi walikubali kuendeleza sherehe walizokuwa wamezianza, wakifanya lile Mordekai alilokuwa amewaandikia. 24Kwa maana Hamani mwana wa Hamedatha Mwagagi, adui wa Wayahudi wote, alikuwa amepanga hila dhidi ya Wayahudi ili kuwaangamiza, na alikuwa amepiga puri (yaani kura) kwa ajili ya maangamizi na uharibifu wao. 25Lakini wakati shauri hilo baya lilipoarifiwa kwa mfalme, alitoa amri iliyoandikwa kwamba mipango mibaya ambayo Hamani ameipanga dhidi ya Wayahudi inapasa imrudie juu ya kichwa chake mwenyewe, na kwamba yeye na wanawe waangikwe mahali pa kunyongea watu. 26(Kwa hiyo siku hizi ziliitwa Purimu, kutokana na neno puri.) Kwa sababu ya kila kitu kilichoandikwa kwenye barua hii na kwa sababu ya yale waliyoyaona na yale yaliyowatokea, 27Wayahudi wakachukua na kuimarisha desturi kwamba wao na wazao wao na wote ambao walijiunga nao wangezishika siku hizi mbili kila mwaka bila kuacha, kwa njia ilivyoelekezwa na kwa wakati wake. 28Siku hizi zinapasa zikumbukwe na kuadhimishwa katika kila kizazi, kila jamaa na katika kila jimbo na kila jiji. Nazo siku hizi za Purimu kamwe zisikome kusherehekewa na Wayahudi, wala kumbukumbu zake zisipotee miongoni mwa wazao wake.
29Basi Malkia Esta binti Abihaili, pamoja na Mordekai Myahudi, waliandika kwa mamlaka yote kuthibitisha barua hii ya pili kuhusu Purimu. 30Naye Mordekai akatuma barua kwa Wayahudi wote katika majimbo mia moja na ishirini na saba (127) ya ufalme wa Ahasuero, barua zenye maneno ya amani na matumaini, 31ili kuimarisha siku hizi za Purimu katika majira yake yaliyowekwa, kama Mordekai Myahudi na Malkia Esta walivyowaamuru, na walivyojiimarisha wenyewe na wazao wao kuhusu nyakati za kufunga na kuomboleza. 32Amri ya Esta ilithibitisha taratibu hizi kuhusu Purimu, nayo ikaandikwa katika kumbukumbu.
Iliyochaguliwa sasa
Esta 9: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapi.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.