Waefeso 3:8-21
Waefeso 3:8-21 NENO
Ingawa mimi ni mdogo kuliko aliye mdogo kabisa miongoni mwa watakatifu wote, nilipewa neema hii: ili niwahubirie watu wa Mataifa kuhusu utajiri usiopimika ulio ndani ya Al-Masihi, na kuweka wazi kwa kila mtu siri hii iliyokuwa imefichwa tangu zamani katika Mungu, aliyeumba vitu vyote. Ili sasa kupitia kwa jumuiya ya waumini, hekima ya Mungu iliyo ya namna nyingi ipate kujulikana kwa watawala na wenye mamlaka katika ulimwengu wa roho, sawasawa na kusudi lake la milele alilolitimiza katika Al-Masihi Isa Bwana wetu. Ndani yake na kupitia kwa imani katika yeye twaweza kumkaribia Mungu kwa uhuru na kwa ujasiri. Kwa hiyo, nawaomba msikate tamaa kwa sababu ya mateso yangu kwa ajili yenu, hayo ni utukufu wenu. Kwa sababu hii nampigia Baba magoti, ambaye ubaba wote wa kila jamaa za mbinguni na za duniani unatokana naye. Namwomba Mungu awaimarishe kwa kuwatia nguvu mioyo yenu kupitia kwa Roho wake Mtakatifu kwa kadiri ya utajiri wa utukufu wake, ili Al-Masihi apate kukaa mioyoni mwenu kupitia kwa imani. Nami ninaomba kwamba mkiwa wenye mizizi tena imara katika msingi wa upendo, mwe na uwezo wa kufahamu pamoja na watakatifu wote jinsi ulivyo upana, urefu, kimo na kina upendo wa Al-Masihi, na kujua upendo huu unaopita fahamu, ili mpate kujazwa na kufikia kipimo cha ukamilifu wote wa Mungu. Basi kwa yeye awezaye kutenda mambo ya ajabu yasiyopimika kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya uweza wake ule utendao kazi ndani yetu, yeye atukuzwe katika jumuiya ya waumini, na katika Al-Masihi Isa kwa vizazi vyote, milele na milele. Amen.