Waefeso 2
2
Kufanywa hai ndani ya Al-Masihi
1Ninyi mlikuwa wafu katika makosa na dhambi zenu, 2ambazo mlizitenda mlipofuata njia za ulimwengu huu na za yule mtawala wa ufalme wa anga, yule roho atendaye kazi sasa ndani ya wale wasiotii. 3Sisi sote pia tuliishi katikati yao hapo zamani, tukitimiza tamaa za asili yetu ya dhambi na kufuata tamaa zake na mawazo yake. Nasi kwa asili tulistahili ghadhabu, kama watu wengine wote. 4Lakini Mungu kwa upendo wake mwingi kwetu sisi, ambaye ni mwingi wa rehema, 5hata tulipokuwa wafu kwa ajili ya makosa yetu, alitufanya tuwe hai pamoja na Al-Masihi Isa, yaani mmeokolewa kwa neema. 6Mungu alitufufua pamoja na Al-Masihi na kutuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho katika Al-Masihi Isa, 7ili katika ulimwengu ujao apate kuonesha wingi wa neema yake isiyolinganishwa, iliyodhihirishwa kwetu kwa wema wake ndani ya Al-Masihi Isa. 8Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kupitia kwa imani, nayo haikutokana na ninyi wenyewe. Hii ni zawadi kutoka kwa Mungu, 9si kwa matendo, ili mtu yeyote asije akajisifu. 10Kwa maana sisi ni kazi ya mikono ya Mungu, tulioumbwa katika Al-Masihi Isa, ili tupate kutenda matendo mema, ambayo Mungu alitangulia kuyaandaa tupate kuishi katika hayo.
Wamoja katika Al-Masihi
11Kwa hiyo kumbukeni kwamba hapo awali ninyi ambao ni watu wa Mataifa kwa kuzaliwa na kuitwa “wasiotahiriwa” na wale wanaojiita “waliotahiriwa” (yaani tohara ifanyikayo katika mwili kwa mikono ya wanadamu), 12kumbukeni kwamba wakati ule mlikuwa mbali na Al-Masihi, mkiwa mmetengwa kutoka jumuiya ya Israeli, na mkiwa wageni katika yale maagano ya ahadi, nanyi hamkuwa na tumaini wala Mungu duniani. 13Lakini sasa katika Al-Masihi Isa, ninyi ambao hapo kwanza mlikuwa mbali na Mungu, sasa mmeletwa karibu kupitia kwa damu ya Al-Masihi.
14Kwa maana yeye mwenyewe ndiye amani yetu, aliyetufanya sisi tuliokuwa vikundi viwili tuwe kikundi kimoja kwa kuvunja kizuizi na kubomoa ule ukuta wa uadui uliokuwa kati yetu, 15kwa kuibatilisha ile sheria pamoja na amri zake na maagizo yake alipoutoa mwili wake, ili apate kufanya ndani yake mtu mmoja mpya badala ya hao wawili, hivyo akifanya amani, 16naye katika mwili huu mmoja awapatanishe wote wawili na Mungu kupitia msalaba, ili kwa huo msalaba akaangamiza uadui wao. 17Alikuja na kuhubiri amani kwenu ninyi mliokuwa mbali, na pia akahubiri amani kwao waliokuwa karibu. 18Kwa maana kupitia kwake sisi sote tunaweza kumkaribia Baba katika Roho mmoja.
19Hivyo basi, ninyi sasa si wageni tena na wapitaji, bali mmekuwa wenyeji pamoja na watakatifu na pia jamaa wa nyumbani mwake Mungu. 20Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Al-Masihi Isa ndiye jiwe kuu la pembeni. 21Ndani yake jengo lote limeshikamanishwa pamoja na kuinuliwa ili kuwa Hekalu takatifu katika Mwenyezi Mungu. 22Katika yeye ninyi nanyi mnajengwa pamoja ili mpate kuwa makao ambayo Mungu anaishi ndani yake kupitia kwa Roho wake Mtakatifu.
Iliyochaguliwa sasa
Waefeso 2: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapi.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.