Waefeso 2:11-16
Waefeso 2:11-16 NENO
Kwa hiyo kumbukeni kwamba hapo awali ninyi ambao ni watu wa Mataifa kwa kuzaliwa na kuitwa “wasiotahiriwa” na wale wanaojiita “waliotahiriwa” (yaani tohara ifanyikayo katika mwili kwa mikono ya wanadamu), kumbukeni kwamba wakati ule mlikuwa mbali na Kristo, mkiwa mmetengwa kutoka jumuiya ya Israeli, na mkiwa wageni katika yale maagano ya ahadi, nanyi hamkuwa na tumaini wala Mungu duniani. Lakini sasa katika Kristo Yesu, ninyi ambao hapo kwanza mlikuwa mbali na Mungu, sasa mmeletwa karibu kupitia kwa damu ya Kristo. Kwa maana yeye mwenyewe ndiye amani yetu, aliyetufanya sisi tuliokuwa vikundi viwili tuwe kikundi kimoja kwa kuvunja kizuizi na kubomoa ule ukuta wa uadui uliokuwa kati yetu, kwa kuibatilisha ile sheria pamoja na amri zake na maagizo yake alipoutoa mwili wake, ili apate kufanya ndani yake mtu mmoja mpya badala ya hao wawili, hivyo akifanya amani, naye katika mwili huu mmoja awapatanishe wote wawili na Mungu kupitia msalaba, ili kwa huo msalaba akaangamiza uadui wao.