Mhubiri 3
3
Kila Jambo Lina Wakati Wake
1 Kuna wakati kwa ajili ya kila jambo,
nayo majira kwa kila tendo chini ya mbingu:
2 wakati wa kuzaliwa na wakati wa kufa,
wakati wa kupanda na wakati wa kungʼoa yaliyopandwa,
3 wakati wa kuua na wakati wa kuponya,
wakati wa kubomoa,
na wakati wa kujenga,
4 wakati wa kulia na wakati wa kucheka,
wakati wa kuomboleza na wakati wa kucheza,
5wakati wa kutawanya mawe na wakati wa kukusanya mawe,
wakati wa kukumbatia na wakati wa kutokumbatia,
6wakati wa kutafuta na wakati wa kupoteza,
wakati wa kuweka na wakati wa kutupa,
7 wakati wa kurarua na wakati wa kushona,
wakati wa kunyamaza na wakati wa kuzungumza,
8wakati wa kupenda na wakati wa kuchukia,
wakati wa vita na wakati wa amani.
9Mfanyakazi anapata faida gani kutokana na taabu yake? 10 Nimeona mzigo Mungu alioweka juu ya wanadamu. 11 Amefanya kila kitu kiwe kizuri kwa wakati wake. Pia ameiweka hiyo milele katika mioyo ya wanadamu, wala hawawezi kutambua kwa kina yale ambayo Mungu amefanya tangu mwanzo hadi mwisho. 12Ninajua kwamba hakuna kitu bora kwa wanadamu kuliko kuwa na furaha na kutenda mema wakati wanapoishi. 13 Tena ni karama ya Mungu kila mtu apate kula na kunywa na kujiburudisha kwa mema katika kazi yake yote. 14 Ninajua kwamba kila kitu anachokifanya Mungu kitadumu milele, hakuna kinachoweza kuongezwa au kupunguzwa. Mungu hufanya hivyo ili watu wamche yeye.
15 Chochote kilichopo kilishakuwepo,
na kitakachokuwepo kimekwishakuwepo kabla;
naye Mungu huyaita yale yaliyopita yarudi tena.
16Pia nikaona kitu kingine tena chini ya jua:
Mahali pa kutolea hukumu,
uovu ulikuwepo,
mahali pa kupatia haki,
uovu ulikuwepo.
17 Nikafikiri moyoni mwangu,
“Mungu atawaleta hukumuni
wote wawili wenye haki na waovu,
kwa maana kutakuwako na wakati kwa ajili ya kila jambo,
wakati kwa ajili ya kila tendo.”
18 Pia nikafikiri, “Kuhusu wanadamu, Mungu huwajaribu ili wajione kwamba wao ni kama wanyama. 19 Hatima ya mwanadamu ni kama ile ya wanyama; wote wana mwisho unaofanana: Jinsi anavyokufa mnyama, ndivyo anavyokufa mwanadamu. Wote wana pumzi inayofanana; mwanadamu hana cha zaidi kuliko mnyama. Kila kitu ni ubatili. 20 Wote huenda mahali panapofanana; wote hutoka mavumbini, mavumbini wote hurudi. 21 Ni nani ajuaye kama roho ya mtu huenda juu na roho ya mnyama hushuka chini ardhini?”
22 Kwa hiyo nikaona kwamba hakuna kitu kilicho bora zaidi kwa mwanadamu kuliko kuifurahia kazi yake, kwa sababu hilo ndilo fungu lake. Kwa maana ni nani awezaye kumrudisha ili aje kuona kile kitakachotendeka baada yake?
Iliyochaguliwa sasa
Mhubiri 3: NEN
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Biblia Takatifu™ Neno™
Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Version™
Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 by Biblica, Inc.
Used with Permission. All Rights Reserved Worldwide.