Kumbukumbu 8:1-9
Kumbukumbu 8:1-9 NEN
Uwe mwangalifu kufuata kila agizo ninalokupa wewe leo, ili mweze kuishi, kuongezeka na mweze kuingia mkamiliki nchi ambayo BWANA aliahidi kwa kiapo kwa baba zenu. Kumbuka jinsi BWANA Mungu wenu alivyowaongoza katika njia yote katika jangwa kwa miaka hii arobaini, kukunyenyekeza na kukujaribu ili ajue lililoko moyoni mwako, kwamba utayashika maagizo yake au la. Alikudhili na kukufanya uone njaa kisha akulishe kwa mana, ambayo wewe wala baba zako hamkuijua, awafundishe kuwa mwanadamu hataishi kwa mkate tu bali kwa kila neno litokalo katika kinywa cha BWANA. Nguo zenu hazikuchakaa wala miguu yenu haikuvimba kwa miaka hii arobaini. Mjue basi ndani ya mioyo yenu kama mtu anavyomwadibisha mwanawe, ndivyo BWANA Mungu wako atawaadibisha ninyi. Shikeni maagizo ya BWANA Mungu wenu mtembee katika njia zake na kumheshimu. Kwa kuwa BWANA Mungu wenu anawaleta katika nchi nzuri, nchi yenye vijito na mabwawa ya maji, yenye chemchemi zinazotiririka mabondeni na katika vilima; nchi yenye ngano na shayiri, mizabibu na mitini, mikomamanga, mafuta ya zeituni na asali; nchi ambayo chakula hakitapungua na hamtakosa chochote; nchi ambayo miamba yake ni chuma na mnaweza kuchimba shaba kutoka kwenye vilima.