Kumbukumbu 32:28-44
Kumbukumbu 32:28-44 NEN
Wao ni taifa lisilo na akili, hakuna busara ndani yao. Laiti wangekuwa na hekima wangefahamu hili, na kutambua mwisho wao utakuwa aje! Mtu mmoja angewezaje kufukuza elfu moja, au wawili kufukuza elfu kumi, kama si kwamba Mwamba wao amewauza, kama si kwamba BWANA amewaacha? Kwa kuwa mwamba wao si kama Mwamba wetu, sawasawa na vile adui zetu wanavyokiri. Mzabibu wao unatoka kwenye mzabibu wa Sodoma, na kutoka kwenye mashamba ya Gomora. Zabibu zake zimejaa sumu, na vishada vyake vimejaa uchungu. Mvinyo wao ni sumu ya nyoka, sumu yenye kufisha ya swila. “Je, hili sikuliweka akiba na kulifungia kwenye vyumba vyangu vya hazina? Ni juu yangu kulipiza kisasi; nitalipiza. Wakati utakapowadia, mguu wao utateleza; siku yao ya maafa ni karibu, na maangamizo yao yanawajia haraka.” BWANA atawahukumu watu wake, na kuwahurumia watumishi wake atakapoona nguvu zao zimekwisha wala hakuna yeyote aliyebaki, mtumwa au aliye huru. Atasema: “Sasa iko wapi miungu yao, mwamba walioukimbilia, miungu wale waliokula mafuta ya dhabihu zao na kunywa mvinyo wa sadaka zao za vinywaji? Wainuke basi, wawasaidie! Wawapeni basi ulinzi! “Tazama basi, Mimi mwenyewe, Mimi Ndiye! Hakuna mungu mwingine ila Mimi. Mimi ninaua na Mimi ninafufua, Mimi nimejeruhi na Mimi nitaponya, wala hakuna awezaye kuokoa kutoka mkononi mwangu. Ninainua mkono wangu kuelekea mbinguni na kusema: Hakika kama niishivyo milele, wakati ninapounoa upanga wangu unaometameta na mkono wangu unapoushika ili kutoa hukumu, nitalipiza kisasi juu ya adui zangu na kuwalipiza wale wanaonichukia. Nitailevya mishale yangu kwa damu, wakati upanga wangu ukitafuna nyama: damu ya waliochinjwa pamoja na mateka, vichwa vya viongozi wa adui.” Furahini, enyi mataifa, pamoja na watu wake, kwa kuwa atailipiza damu ya watumishi wake, atalipiza kisasi juu ya adui zake na kufanya upatanisho kwa ajili ya nchi na watu wake. Mose na Yoshua mwana wa Nuni wakaja, wakanena maneno yote ya wimbo watu wakiwa wanasikia.