Kumbukumbu 31:1-13
Kumbukumbu 31:1-13 NEN
Kisha Mose akaenda akasema maneno haya kwa Waisraeli wote: “Sasa nina miaka mia moja na ishirini nami siwezi tena kuwaongoza. BWANA ameniambia, ‘Hutavuka Yordani.’ BWANA Mungu wenu, yeye mwenyewe atavuka mbele yenu. Ataangamiza mataifa haya mbele yenu, nanyi mtaimiliki nchi yao. Pia Yoshua atavuka mbele yenu, kama BWANA alivyosema. Naye BWANA atawafanyia watu hao kile alichowafanyia Sihoni na Ogu, wafalme wa Waamori, ambao aliwaangamiza pamoja na nchi yao. BWANA atawakabidhi kwenu, nanyi lazima mwatendee yale yote niliyowaamuru. Kuweni imara na moyo wa ushujaa. Msiogope wala msifadhaike kwa sababu yao, kwa kuwa BWANA Mungu wenu anakwenda pamoja nanyi; kamwe hatawaacha wala hatawatupa ninyi.” Kisha Mose akamwita Yoshua na akamwambia mbele ya Israeli wote, “Uwe imara na moyo wa ushujaa, kwa kuwa ni lazima uende na watu hawa katika nchi ile BWANA aliyowaapia baba zao kuwapa, nawe ni lazima uwagawie kama urithi wao. BWANA mwenyewe atakutangulia naye atakuwa pamoja nawe; kamwe hatakuacha wala hatakutupa. Usiogope, wala usifadhaike.” Kwa hiyo Mose akaandika sheria hii na kuwapa makuhani, wana wa Lawi, waliochukua Sanduku la Agano la BWANA na wazee wote wa Israeli. Kisha Mose akawaamuru, akasema: “Mwishoni mwa kila miaka saba, katika mwaka wa kufuta madeni, wakati wa Sikukuu ya Vibanda, Waisraeli wote wanapokuja mbele za BWANA Mungu wenu mahali atakapopachagua, utasoma sheria hii mbele yao masikioni mwao. Kusanya watu wote, wanaume, wanawake, watoto na wageni wanaoishi katika miji yenu, ili waweze kusikia na kujifunza kumcha BWANA Mungu wenu na kufuata kwa bidii maneno yote ya sheria hii. Watoto wao, ambao hawaijui sheria hii, lazima waisikie na kujifunza kumcha BWANA Mungu wenu kwa muda mtakaoishi katika nchi mnayovuka Yordani kuimiliki.”