Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kumbukumbu 27

27
Madhabahu katika Mlima Ebali
1Musa na wazee wa Israeli wakawaagiza watu: “Yashikeni maagizo haya yote ninayowaagiza leo. 2Mtakapokuwa mmevuka Mto Yordani na kuingia katika nchi anayowapa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, msimamishe mawe makubwa na myapake chokaa. 3Andikeni juu yake maneno yote ya sheria hii wakati mtakapokuwa mmevuka na kuingia katika nchi anayowapa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, nchi inayotiririka maziwa na asali, kama vile Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zenu, alivyowaahidi. 4Mtakapokuwa mmevuka Yordani, simamisheni mawe haya juu ya Mlima Ebali, kama ninavyowaagiza leo, na myapake chokaa. 5Huko mjengeeni Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, madhabahu, madhabahu ya mawe. Msitumie kifaa chochote cha chuma juu yake. 6Jengeni madhabahu ya Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, kwa mawe ya shambani, na mtoe sadaka za kuteketezwa juu yake kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu. 7Toeni sadaka za amani juu yake, mkizila na kufurahia mbele za Mwenyezi Mungu, Mungu wenu. 8Nanyi mtaandika maneno yote ya sheria hii kwa wazi sana juu ya mawe haya ambayo mmesimamisha.”
Laana kutoka Mlima Ebali
9Kisha Musa na makuhani, ambao ni Walawi, wakawaambia Israeli wote, “Nyamaza ee Israeli, sikiliza! Sasa umekuwa taifa la Mwenyezi Mungu, Mungu wako. 10Mtii Mwenyezi Mungu, Mungu wako, na kufuata amri zake na maagizo ninayokupa leo.”
11Siku ile ile Musa akawaagiza watu:
12Mtakapovuka Mto Yordani, makabila haya yatasimama juu ya Mlima Gerizimu kubariki watu: Simeoni, Lawi, Yuda, Isakari, Yusufu na Benyamini. 13Makabila haya yatasimama juu ya Mlima Ebali kwa kutamka laana: Reubeni, Gadi, Asheri, Zabuloni, Dani na Naftali.
14Nao Walawi watawasomea watu wote wa Israeli kwa sauti kubwa:
15“Alaaniwe mtu afanyaye sanamu ya kuchonga au mwenye kusubu sanamu, kitu ambacho ni chukizo kwa Mwenyezi Mungu, kazi ya mikono ya fundi stadi, na kuisimamisha kwa siri.”
Kisha watu wote watasema, “Amen!”
16“Alaaniwe mtu amdharauye baba yake na mama yake.”
Kisha watu wote watasema, “Amen!”
17“Alaaniwe mtu asogezaye jiwe la mpaka wa jirani yake.”
Kisha watu wote watasema, “Amen!”
18“Alaaniwe mtu ampotoshaye kipofu njiani.”
Kisha watu wote watasema, “Amen!”
19“Alaaniwe mtu apotoshaye haki ya mgeni, yatima au mjane.”
Kisha watu wote watasema, “Amen!”
20“Alaaniwe mtu akutanaye kimwili na mke wa baba yake, kwa maana anadharau malazi ya baba yake.”
Kisha watu wote watasema, “Amen!”
21“Alaaniwe mtu akutanaye kimwili na mnyama yeyote.”
Kisha watu wote watasema, “Amen!”
22“Alaaniwe mtu akutanaye kimwili na dada yake, binti ya baba yake au binti ya mama yake.”
Kisha watu wote watasema, “Amen!”
23“Alaaniwe mtu akutanaye kimwili na mama mkwe wake.”
Kisha watu wote watasema, “Amen!”
24“Alaaniwe mtu amuuaye jirani yake kwa siri.”
Kisha watu wote watasema, “Amen!”
25“Alaaniwe mtu apokeaye rushwa ili kumuua mtu asiye na hatia.”
Kisha watu wote watasema, “Amen!”
26“Alaaniwe mtu yule ambaye hatashikilia maneno ya sheria hii kwa kuyatekeleza.”
Kisha watu wote watasema, “Amen!”

Iliyochaguliwa sasa

Kumbukumbu 27: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia