Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kumbukumbu 13

13
Kuabudu miungu mingine
1Kama nabii, au yule anayetabiri kupitia ndoto, akijitokeza miongoni mwenu na akawatangazia ishara ya miujiza na ajabu, 2ikiwa ishara au ajabu ya aliyozungumza ikatokea, naye akasema, “Na tufuate miungu mingine” (miungu ambayo hamjaifahamu) “na tuiabudu,” 3kamwe msiyasikilize maneno ya nabii wala mwota ndoto huyo. Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anawajaribu kuangalia kama mnampenda kwa moyo wote na kwa roho yote. 4Ni Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, ambaye mnapaswa kumfuata tena ni yeye mnapaswa kumheshimu. Shikeni maagizo yake na kumtii, mtumikieni na kushikamana naye. 5Huyo nabii au mwota ndoto lazima auawe, kwa sababu amehubiri uasi dhidi ya Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, ambaye aliwatoa kutoka nchi ya Misri na kuwakomboa kutoka nchi ya utumwa; amejaribu kuwageuza kutoka njia ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, aliwaagiza mfuate. Ni lazima mwondoe uovu miongoni mwenu.
6Kama ndugu yako hasa, au mwanao au binti yako, au mke umpendaye, au rafiki yako wa karibu sana akikushawishi kwa siri, akisema, “Na twende tukaabudu miungu mingine” (miungu ambayo ninyi wala baba zenu hamkuifahamu, 7miungu ya watu wanaowazunguka, ikiwa karibu au mbali, kutoka mwisho mmoja wa nchi hadi mwingine), 8usikubali wala usimsikilize. Usimhurumie! Usimwache wala usimkinge. 9Hakika ni lazima auawe. Ni lazima mkono wako uwe wa kwanza katika kumuua kisha mikono ya watu wengine wote. 10Mpigeni kwa mawe hadi afe, kwa sababu alijaribu kuwageuza mtoke kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, ambaye aliwatoa Misri, kutoka nchi ya utumwa. 11Kisha Israeli wote watasikia na kuogopa, wala hakuna mmoja miongoni mwenu atakayefanya uovu tena.
12Mkisikia ikisemwa kwamba moja ya miji ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anawapa mkae ndani yake 13kuna wanaume waovu wameinuka miongoni mwenu na wamewapotosha watu wa mji, wakisema, “Twendeni tukaabudu miungu mingine” (miungu ambayo hamkuifahamu), 14ndipo itakubidi kuuliza, kupima na kuchunguza kwa makini. Kama ni kweli, tena ikihakikishwa kwamba jambo hili linalochukiza limefanyika miongoni mwenu, 15kwa hakika ni lazima mwaue kwa upanga wale wote wanaoishi katika mji ule. Uharibuni kabisa, pamoja na watu wake na mifugo yake. 16Kusanyeni nyara zote za mji katika uwanja wa wazi na kuuchoma mji kabisa pamoja na nyara zake zote kuwa sadaka ya kuteketezwa kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu. Utabaki kuwa magofu milele na hautajengwa tena. 17Hakuna kimoja kati ya vitu vilivyolaaniwa kitakachokutwa mikononi mwenu, ili Mwenyezi Mungu ageuze hasira yake kali. Atawahurumia na kuwa na rehema kwenu pia kuongeza idadi yenu, kama alivyowaahidi baba zenu, 18kwa sababu mnamtii Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, mkizishika amri zake zote ninazowapa leo na kufanya lililo jema machoni pake.

Iliyochaguliwa sasa

Kumbukumbu 13: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia