Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Danieli 9:20-27

Danieli 9:20-27 NENO

Basi, nilipokuwa bado nikinena na kuomba, nikiungama dhambi yangu na dhambi ya watu wangu Israeli, na nikifanya maombi yangu kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wangu, kwa ajili ya mlima wake mtakatifu, wakati nilipokuwa bado katika maombi, Jibraili, yule mtu niliyekuwa nimemwona katika maono hapo awali, alinijia kwa kasi karibu wakati wa kutoa dhabihu ya jioni. Akanielimisha na kuniambia, “Danieli, sasa nimekuja kukupa akili na ufahamu. Mara ulipoanza kuomba, jibu lilitolewa, ambalo nimekuja kukupasha habari, kwa maana wewe unapendwa sana. Kwa hiyo, tafakari ujumbe huu na uelewe maono haya: “Majuma sabini yameamriwa kwa ajili ya watu wako na kwa ajili ya mji wako mtakatifu, ili kumaliza makosa, kukomesha dhambi, kufanya upatanisho kwa ajili ya uovu, kuleta haki ya milele, kutia muhuri maono na unabii, na pia kumpaka mafuta yeye aliye mtakatifu sana. “Ujue na kuelewa hili: Tangu kutolewa kwa amri ya kuutengeneza na kuujenga upya Yerusalemu hadi kuja kwa Mpakwa mafuta, aliye mtawala, kutakuwa na majuma saba, na majuma sitini na mawili. Barabara zitajengwa tena pamoja na mahandaki, lakini katika wakati wa taabu. Baada ya majuma sitini na mawili, Mpakwa Mafuta atakatiliwa mbali, wala hatabaki na kitu. Watu wa mtawala atakayekuja watauharibu mji pamoja na mahali patakatifu. Mwisho utakuja kama mafuriko: Vita vitaendelea hadi mwisho, nao ukiwa umeamriwa. Mtawala huyo atathibitisha agano na watu wengi kwa juma moja. Katikati ya juma hilo atakomesha dhabihu na sadaka. Mahali pa dhabihu katika Hekalu, atasimamisha chukizo la uharibifu, hadi mwisho ulioamriwa utakapomiminwa juu yake yeye aletaye uharibifu.”