Danieli 8:15-27
Danieli 8:15-27 NENO
Mimi Danieli nilipokuwa ninaangalia maono na kujaribu kuelewa, mbele yangu alisimama mmoja aliyefanana na mwanadamu. Kisha nikasikia sauti ya mwanadamu kutoka Mto Ulai ikiita, “Jibraili, mwambie mtu huyu maana ya maono haya.” Alipokuwa akikaribia pale nilipokuwa nimesimama, niliogopa, nikaanguka kifudifudi. Akaniambia, “Mwana wa mwanadamu, fahamu kuwa maono haya yanahusu siku za mwisho.” Alipokuwa akinena nami, nilikuwa katika usingizi mzito, huku nimelala kifudifudi. Ndipo aliponigusa na kunisimamisha wima. Akaniambia, “Nitakuambia yale yatakayotokea baadaye wakati wa ghadhabu, kwa sababu maono haya yanahusu wakati wa mwisho ulioamriwa. Kondoo dume mwenye pembe mbili ambaye ulimwona anawakilisha wafalme wa Umedi na Uajemi. Yule beberu mwenye manyoya mengi ni mfalme wa Uyunani, nayo ile pembe ndefu katikati ya macho yake ni mfalme wa kwanza. Zile pembe nne zilizoota badala ya ile pembe iliyovunjika zinawakilisha falme nne ambazo zitatokea kutoka taifa lake, lakini hakuna hata mmoja utakaokuwa na nguvu kama ile pembe iliyovunjika. “Katika sehemu ya mwisho ya utawala wao, waasi watakapokuwa waovu kabisa, atainuka mfalme mwenye uso mkali, aliye stadi wa hila. Atakuwa na nguvu nyingi, lakini si kwa uwezo wake mwenyewe. Atasababisha uharibifu wa kutisha, na atafanikiwa kwa chochote anachofanya. Atawaangamiza watu maarufu na watu watakatifu. Atasababisha udanganyifu ustawi, naye atajihesabu mwenyewe kuwa bora kuliko wote. Wakati watajisikia kuwa salama, atawaangamiza wengi, na kushindana na Mkuu wa wakuu. Lakini ataangamizwa, isipokuwa si kwa uwezo wa mwanadamu. “Maono kuhusu jioni na asubuhi ambayo umepewa ni kweli, lakini yatie muhuri maono haya, kwa maana yanahusu nyakati za baadaye sana.” Mimi Danieli nilikuwa nimechoka sana, na nikalala nikiwa mgonjwa kwa siku kadhaa. Ndipo nikaamka, nikaendelea na shughuli za mfalme. Nilifadhaishwa na maono hayo; sikuweza kuyaelewa.