Danieli 6:1-16
Danieli 6:1-16 NENO
Ilimpendeza Dario kuteua wakuu mia moja na ishirini kutawala katika ufalme wake wote, pamoja na wasimamizi watatu juu yao, Danieli akiwa mmoja wao. Wakuu walitoa hesabu kwa wasimamizi hao ili mfalme asipate hasara. Basi Danieli alijidhihirisha miongoni mwa wasimamizi na wakuu kwa sifa zake za kipekee, hata mfalme akapanga kumweka juu ya ufalme wote. Walipofahamu hilo, wasimamizi na wakuu wakajaribu kutafuta sababu za kumshtaki Danieli kuhusu usimamizi wake wa shughuli za serikali, lakini hawakuweza kufanikiwa. Hawakuweza kupata kosa kwake, kwa sababu alikuwa mwaminifu, wala hakupatikana na upotovu au uzembe. Mwishoni watu hawa wakasema, “Kamwe hatutapata msingi wa mashtaka dhidi ya huyu Danieli, isipokuwa iwe inahusiana na sheria ya Mungu wake.” Basi wasimamizi na wakuu wakaingia kwa mfalme kama kikundi, wakasema, “Ee Mfalme Dario, uishi milele! Wasimamizi wa ufalme, wasaidizi, wakuu, washauri na watawala wote wamekubaliana kwamba mfalme atoe sheria na kukazia amri kuwa yeyote atakayetoa dua kwa mungu au mwanadamu katika muda huu wa siku thelathini zijazo, isipokuwa kwako wewe, ee mfalme, atupwe ndani ya tundu la simba. Sasa, ee mfalme, toa amri na uiandike ili isiweze kubadilishwa: kulingana na sheria za Wamedi na Waajemi, ambazo haziwezi kubatilishwa.” Hivyo Mfalme Dario akaiweka amri hiyo katika maandishi. Basi Danieli alipofahamu kuwa amri ile imetangazwa, alienda nyumbani mwake kwenye chumba chake cha ghorofani, ambako madirisha yalifunguka kuelekea Yerusalemu. Akapiga magoti na kuomba mara tatu kwa siku, akimshukuru Mungu wake, kama alivyokuwa akifanya awali. Ndipo watu hawa wakaenda kama kikundi na kumkuta Danieli akiomba na kumsihi Mungu kwa ajili ya msaada. Basi wakaenda kwa mfalme na kusema naye kuhusu amri ya mfalme: “Je, hukutangaza amri kwamba kwa muda huu wa siku thelathini zijazo mtu ambaye atamwomba mungu au mwanadamu yeyote isipokuwa wewe, ee mfalme, angetupwa ndani ya tundu la simba?” Mfalme akajibu, “Amri ndivyo ilivyo, kulingana na sheria za Wamedi na Waajemi, ambazo haziwezi kubatilishwa.” Ndipo wakamwambia mfalme, “Danieli, ambaye ni mmoja wa mahamisho kutoka Yuda, hakuheshimu, ee mfalme, wala hajali amri uliyoiweka kwa maandishi. Bado anaomba mara tatu kwa siku.” Mfalme aliposikia hili, akahuzunika mno. Akakusudia kumwokoa Danieli, hivyo akafanya kila jitihada ya kumwokoa hadi jua likatua. Ndipo wale watu wakamwendea mfalme kama kikundi na kumwambia, “Ee mfalme, kumbuka kwamba kulingana na sheria ya Wamedi na Waajemi, hakuna amri wala sheria ambayo mfalme ameitoa inayoweza kubadilishwa.” Basi mfalme akatoa amri, nao wakamleta Danieli, wakamtupa ndani ya tundu la simba. Mfalme akamwambia Danieli, “Mungu wako unayemtumikia daima na akuokoe!”