Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Danieli 12:5-13

Danieli 12:5-13 NENO

Ndipo mimi Danieli nikaangalia, nako mbele yangu walisimama wengine wawili, mmoja katika ukingo huu wa mto, na mwingine ukingo wa pili wa mto. Mmoja wao akamwambia yule mtu aliyevaa nguo za kitani, aliyekuwa juu ya maji ya mto, “Je, itachukua muda gani kabla mambo haya ya kushangaza hayajatimizwa?” Kisha mtu yule aliyevaa nguo za kitani, aliyekuwa juu ya maji ya mto, akainua mkono wake wa kuume na mkono wake wa kushoto kuelekea mbinguni, nami nikamsikia akiapa kwa jina lake yeye aishiye milele, akisema, “Itakuwa wakati, nyakati mbili, na nusu wakati. Nguvu za watu watakatifu zitakapokuwa zimevunjwa kabisa, ndipo mambo haya yote yatakapotimizwa.” Nilisikia, lakini sikuelewa. Kwa hiyo nikauliza, “Bwana wangu, matokeo ya haya yote yatakuwa nini?” Akajibu, “Danieli, nenda zako, kwa sababu maneno haya yamefungwa na kutiwa muhuri hadi wakati wa mwisho. Wengi watatakaswa, na kuondolewa mawaa na kufanywa safi, lakini waovu wataendelea kuwa waovu. Hakuna mmoja wa waovu atakayefahamu, lakini wale wenye hekima watafahamu. “Tangu wakati ule wa kukomeshwa kwa dhabihu ya kila siku, na kuanzishwa kwa chukizo la uharibifu, kutakuwepo siku elfu moja na mia mbili na tisini (1,290). Kubarikiwa ni yule atakayevumilia hadi kufikia mwisho wa hizo siku elfu moja mia tatu na thelathini na tano (1,335). “Lakini wewe, nenda zako hadi mwisho. Utapumzika, nawe mwisho wa hizo siku utafufuka ili kuupokea urithi uliowekewa.”