Amosi 5:10-17
Amosi 5:10-17 NEN
mnamchukia yule akemeaye mahakamani, na kumdharau yule ambaye husema kweli. Mnamgandamiza maskini na kumlazimisha awape nafaka. Kwa hiyo, ingawa mmejenga majumba ya mawe ya fahari, hamtaishi ndani yake; ingawa mmepanda mashamba mazuri ya mizabibu, hamtakunywa divai yake. Kwa kuwa ninajua hesabu ya makosa yenu na ukubwa wa dhambi zenu. Mmewaonea wenye haki na kupokea rushwa na kuzuia haki ya maskini mahakamani. Kwa hiyo mtu mwenye busara hunyamaza kimya nyakati kama hizo, kwa kuwa nyakati ni mbaya. Tafuteni mema, wala si mabaya, ili mpate kuishi. Ndipo BWANA Mungu Mwenye Nguvu Zote atakuwa pamoja nanyi, kama msemavyo yupo nanyi. Yachukieni maovu, yapendeni mema; dumisheni haki mahakamani. Yamkini BWANA Mungu Mwenye Nguvu Zote atawahurumia mabaki ya Yosefu. Kwa hiyo hili ndilo Bwana, BWANA Mungu Mwenye Nguvu Zote, asemalo: “Kutakuwepo maombolezo katika barabara zote na vilio vya uchungu katika njia kuu zote. Wakulima wataitwa kuja kulia, na waombolezaji waje kuomboleza. Kutakuwepo kuomboleza katika mashamba yote ya mizabibu, kwa kuwa nitapita katikati yenu,” asema BWANA.