Amosi 5:1-9
Amosi 5:1-9 NENO
Sikia neno hili, ee nyumba ya Israeli, ombolezo hili ninalifanya kuwahusu ninyi: “Bikira Israeli ameanguka, kamwe hatainuka tena, ameachwa pweke katika nchi yake, hakuna yeyote wa kumwinua.” Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: “Mmoja wa miji yako utakapopeleka watu elfu moja vitani kwa ajili ya Israeli, mia moja tu watarudi; wakati mji utakapopeleka mia moja, kumi tu ndio watarudi hai.” Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu kwa nyumba ya Israeli: “Nitafuteni mpate kuishi; msitafute Betheli, msiende Gilgali, msisafiri kwenda Beer-Sheba. Kwa maana kwa hakika Gilgali itaenda uhamishoni, na Betheli itafanywa kuwa ubatili.” Mtafuteni Mwenyezi Mungu mpate kuishi, au atafagia nyumba ya Yusufu kama moto; utawateketeza, nayo Betheli haitakuwa na yeyote wa kuuzima. Ninyi ambao mnageuza haki kuwa uchungu na kuiangusha haki chini (yeye ambaye alifanya Kilimia na Orioni, ambaye hugeuza giza kuwa mapambazuko na mchana kuwa usiku, ambaye huyaita maji ya bahari na kuyamwaga juu ya nchi: Mwenyezi Mungu ndilo jina lake; yeye hufanya maangamizi kwenye ngome na kufanya mji uliozungushiwa ngome kuwa ukiwa)