Matendo 9:10-18
Matendo 9:10-18 NEN
Huko Dameski alikuwepo mwanafunzi mmoja jina lake Anania. Bwana alimwita katika maono, “Anania!” Akajibu, “Mimi hapa Bwana.” Bwana akamwambia, “Ondoka uende katika barabara iitwayo Nyofu ukaulize katika nyumba ya Yuda mtu kutoka Tarso, jina lake Sauli, kwa maana wakati huu anaomba, katika maono amemwona mtu aitwaye Anania akija na kuweka mikono juu yake ili apate kuona tena.” Anania akajibu, “Bwana, nimesikia kutoka kwa watu wengi habari nyingi kuhusu mtu huyu na madhara yote aliyowatendea watakatifu wako huko Yerusalemu. Naye amekuja hapa Dameski akiwa na mamlaka kutoka kwa viongozi wa makuhani ili awakamate wote wanaotaja jina lako.” Lakini Bwana akamwambia Anania, “Nenda! Mtu huyu ni chombo changu kiteule nilichokichagua, apate kulichukua Jina langu kwa watu wa Mataifa na wafalme wao na mbele ya watu wa Israeli. Nami nitamwonyesha jinsi impasavyo kuteseka kwa ajili ya Jina langu.” Kisha Anania akaenda kwenye ile nyumba, akaingia ndani. Akaweka mikono yake juu ya Sauli akasema, “Ndugu Sauli, Bwana Yesu aliyekutokea njiani amenituma kwako ili upate kuona tena na ujazwe Roho Mtakatifu.” Ghafula vitu kama magamba vikaanguka chini, kutoka machoni mwa Sauli, akapata kuona tena. Akasimama, akabatizwa.