Matendo 8:26-34
Matendo 8:26-34 NEN
Basi malaika wa Bwana akamwambia Filipo, “Nenda upande wa kusini kwenye ile barabara itokayo Yerusalemu kuelekea Gaza ambayo ni jangwa.” Hivyo akaondoka. Akiwa njiani akakutana na towashi wa Kushi, aliyekuwa afisa mkuu, mwenye mamlaka juu ya hazina zote za Kandake, Malkia wa Kushi. Huyu towashi alikuwa amekwenda Yerusalemu ili kuabudu, naye akiwa njiani kurudi nyumbani alikuwa ameketi garini mwake akisoma kitabu cha nabii Isaya. Roho Mtakatifu akamwambia Filipo, “Nenda kwenye lile gari ukae karibu nalo.” Ndipo Filipo akakimbilia lile gari na kumsikia yule mtu anasoma kitabu cha nabii Isaya. Filipo akamuuliza, “Je, unaelewa hayo usomayo?” Yule towashi akasema, “Nitawezaje kuelewa mtu asiponifafanulia?” Hivyo akamkaribisha Filipo ili apande na kuketi pamoja naye. Huyu towashi alikuwa anasoma fungu hili la Maandiko: “Aliongozwa kama kondoo aendaye machinjoni, kama mwana-kondoo anyamazavyo mbele yake yule amkataye manyoya, hivyo hakufungua kinywa chake. Katika kufedheheshwa kwake alinyimwa haki yake. Nani awezaye kueleza juu ya kizazi chake? Kwa maana maisha yake yaliondolewa kutoka duniani.” Yule towashi akamuuliza Filipo, “Tafadhali niambie, nabii huyu anena habari zake mwenyewe au habari za mtu mwingine?”