Matendo 7:37-53
Matendo 7:37-53 NENO
“Huyu ndiye yule Musa aliyewaambia Waisraeli, ‘Mungu atawainulia nabii kama mimi kutoka miongoni mwa ndugu zenu wenyewe.’ Huyu ndiye yule Musa aliyekuwa katika kusanyiko huko jangwani, ambaye malaika alisema naye pamoja na baba zetu kwenye Mlima Sinai, naye akapokea maneno yaliyo hai ili atupatie. “Lakini baba zetu walikataa kumtii Musa, badala yake wakamkataa na kuielekeza mioyo yao Misri tena. Wakamwambia Haruni, ‘Tufanyie miungu itakayotuongoza, kwa maana mtu huyu Musa aliyetutoa nchi ya Misri, hatujui yaliyompata.’ Huu ni ule wakati walitengeneza sanamu katika umbo la ndama, wakailetea sadaka kufanya maadhimisho kwa ajili ya kile kitu walichokitengeneza kwa mikono yao wenyewe. Ndipo Mungu akageuka, akawaachia waabudu jeshi lote la mbinguni, kama ilivyoandikwa katika Kitabu cha Manabii: “ ‘Je, mliniletea dhabihu na sadaka kwa miaka arobaini kule jangwani, ee nyumba ya Israeli? La, ninyi mliinua madhabahu ya Moleki, na nyota ya mungu wenu Refani, vinyago mlivyotengeneza ili kuviabudu. Kwa hiyo nitawapeleka mbali’ kuliko Babeli. “Baba zetu walikuwa na lile Hema la Ushuhuda huko jangwani, ambalo lilitengenezwa kama Mungu alivyomwelekeza Musa, kulingana na kielelezo alichokiona. Baada ya kupokea Hema, baba zetu waliingia nalo walipokuja na Yoshua wakati walimiliki nchi, Mungu alipoyafukuza mataifa mbele yao. Nalo lilidumu katika nchi hadi wakati wa Daudi, ambaye alipata kibali kwa Mungu, naye akaomba kwamba ampatie Mungu wa Yakobo maskani. Lakini Sulemani ndiye aliyemjengea Mungu nyumba. “Hata hivyo, Yeye Aliye Juu Sana hakai kwenye nyumba zilizojengwa kwa mikono ya wanadamu. Kama nabii alivyosema: “ ‘Mbingu ni kiti changu cha enzi, nayo dunia ni mahali pa kuweka miguu yangu. Mtanijengea nyumba ya namna gani? asema Mwenyezi Mungu. Au mahali pangu pa kupumzikia patakuwa wapi? Je, mkono wangu haukuumba vitu hivi vyote?’ “Enyi watu wenye shingo ngumu, msiotahiriwa mioyo wala masikio, daima hamwachi kumpinga Roho wa Mungu, kama walivyofanya baba zenu. Je, kuna nabii gani ambaye baba zenu hawakumtesa? Waliwaua wale waliotabiri habari za kuja kwake yule Mwenye Haki. Nanyi sasa mmekuwa wasaliti wake na wauaji. Ninyi ndio mlipokea sheria zilizoletwa kwenu na malaika, lakini hamkuzitii.”