Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 5:12-21

Matendo 5:12-21 NEN

Mitume wakafanya ishara nyingi na miujiza miongoni mwa watu. Walioamini wote walikuwa wakikusanyika katika ukumbi wa Solomoni. Hakuna mtu mwingine aliyethubutu kuambatana nao ijapokuwa waliheshimiwa sana na watu. Hata hivyo, waliomwamini Bwana wakazidi kuongezeka, wanaume na wanawake. Hata wakawa wanawaleta wagonjwa na kuwalaza kwenye magodoro na kwenye vitanda barabarani ili yamkini Petro akipita kivuli chake kiwaguse baadhi yao. Pia watu wakakusanyika kutoka miji iliyokuwa karibu na Yerusalemu, wakileta wagonjwa na watu walioteswa na pepo wachafu. Hao wote wakaponywa. Kisha kuhani mkuu na wenzake wote waliokuwa pamoja naye, waliokuwa wa kundi la Masadukayo, wakajawa na wivu. Wakawakamata mitume na kuwatia gerezani. Lakini wakati wa usiku, malaika wa Bwana akaja, akafungua milango ya gereza na akawatoa nje. Akawaambia, “Nendeni, mkasimame Hekaluni mkawaambie watu maneno yote ya uzima huu mpya.” Waliposikia haya wakaenda Hekaluni alfajiri wakaendelea kufundisha watu. Kuhani mkuu na wale waliokuwa pamoja nao walipowasili, alikusanya baraza na wazee wote wa Israeli wakatuma wale mitume waletwe kutoka gerezani.