Matendo 4
4
Petro na Yohana mbele ya Baraza
1Petro na Yohana walipokuwa wakisema na watu, makuhani, mkuu wa walinzi wa Hekalu na Masadukayo#4:1 Kundi la kidini la Wayahudi; waliamini kwamba hakuna ufufuo, wala hakuna malaika au roho. wakawajia, 2huku wakiwa wamekasirika sana kwa sababu mitume walikuwa wanawafundisha watu na kuhubiri kwamba kuna ufufuo wa wafu ndani ya Isa. 3Wakawakamata Petro na Yohana na kuwafunga gerezani hadi kesho yake kwa kuwa ilikuwa jioni. 4Lakini wengi waliosikia lile neno waliamini, idadi yao ilikuwa yapata wanaume elfu tano.
5Kesho yake, viongozi wa Wayahudi, wazee na walimu wa Torati walikusanyika Yerusalemu. 6Walikuwemo kuhani mkuu Anasi, Kayafa, Yohana, Iskanda, na wengi wa jamaa ya kuhani mkuu. 7Baada ya kuwasimamisha Petro na Yohana katikati yao, wakawauliza, “Ni kwa uwezo gani au kwa jina la nani mmefanya jambo hili?”
8Petro, akiwa amejawa na Roho Mtakatifu wa Mungu, akajibu, “Enyi watawala na wazee wa watu, 9kama leo tukihojiwa kwa habari ya mambo mema aliyotendewa yule kiwete na kuulizwa jinsi alivyoponywa, 10ijulikane kwenu nyote na kwa watu wote wa Israeli kwamba: Ni kwa jina la Isa Al-Masihi wa Nasiri, ambaye ninyi mlimsulubisha lakini Mungu akamfufua kutoka kwa wafu, kwa jina hilo mtu huyu anasimama mbele yenu akiwa mzima kabisa. 11Huyu ndiye
“ ‘jiwe ambalo ninyi wajenzi mlilikataa,
ambalo limekuwa jiwe kuu la pembeni.’#4:11 Zaburi 118:22
12Wala hakuna wokovu katika mwingine yeyote, kwa maana hakuna jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu linalopasa kutuokoa.”
Ujasiri wa Petro na Yohana washangaza watu
13Viongozi na wazee walipoona ujasiri wa Petro na Yohana, na kujua ya kuwa walikuwa watu wa kawaida, wasio na elimu, walishangaa sana, wakatambua kwamba hawa watu walikuwa na Isa. 14Lakini kwa kuwa walikuwa wanamwona yule kiwete aliyeponywa amesimama pale pamoja nao, hawakuweza kusema lolote kuwapinga. 15Wakawaamuru watoke nje ya Baraza la Wayahudi#4:15 Baraza la Wayahudi ina maana ya Sanhedrin ambalo lilikuwa baraza la juu kabisa la utawala wa Kiyahudi; liliundwa na wazee 70 pamoja na kuhani mkuu., ili wasemezane jambo hilo wao wenyewe. 16Wakaulizana, “Tuwafanyie nini watu hawa? Hatuwezi kukanusha muujiza huu mkubwa walioufanya, ambao ni dhahiri kwa kila mtu Yerusalemu. 17Lakini ili kuzuia jambo hili lisiendelee kuenea zaidi kwa watu, ni lazima tuwaonye watu hawa ili wasiseme tena na mtu yeyote kwa jina la Isa.”
18Kisha wakawaita tena ndani na kuwaamuru wasiseme wala kufundisha kamwe kwa hili jina la Isa.
Imetupasa kumtii Mwenyezi Mungu kuliko wanadamu
19Lakini Petro na Yohana wakajibu, “Amueni ninyi wenyewe iwapo ni haki mbele za Mungu kuwatii ninyi kuliko kumtii Mungu. 20Lakini sisi hatuwezi kuacha kusema yale tuliyoyaona na kuyasikia.”
21Baada ya vitisho vingi, wakawaachia waende zao. Hawakuona njia yoyote ya kuwaadhibu, kwa sababu ya watu, kwa kuwa watu wote walikuwa wakimsifu Mungu kwa kile kilichokuwa kimetukia. 22Kwa kuwa umri wa yule mtu aliyekuwa ameponywa kwa muujiza ulikuwa zaidi ya miaka arobaini.
Maombi ya waumini
23Punde Petro na Yohana walipoachiliwa, walirudi kwa waumini wenzao wakawaeleza waliyoambiwa na viongozi wa makuhani na wazee. 24Watu waliposikia hayo, wakapaza sauti zao, wakamwomba Mungu kwa pamoja, wakisema, “Bwana Mungu Mwenyezi, uliyeziumba mbingu na nchi na bahari, na vitu vyote vilivyomo. 25Wewe ulinena kwa Roho wa Mungu kupitia kwa kinywa cha baba yetu Daudi, mtumishi wako, ukasema:
“ ‘Mbona mataifa wanaghadhibika,
na makabila ya watu kuwaza ubatili?
26Wafalme wa dunia wamejipanga,
na watawala wanakusanyika pamoja
dhidi ya Mwenyezi Mungu
na dhidi ya Mpakwa Mafuta wake.’#4:26 Zaburi 2:1, 2
27Ni kweli Herode na Pontio Pilato, pamoja na watu wa Mataifa na Waisraeli, walikusanyika katika mji huu kupanga njama dhidi ya mwanao mtakatifu Isa, uliyempaka mafuta. 28Wakafanya yale uweza wako na mapenzi yako yalikusudia yatokee tangu zamani. 29Sasa, Mwenyezi Mungu, angalia vitisho vyao na utuwezeshe sisi watumishi wako kulinena neno lako kwa ujasiri mkuu. 30Nyoosha mkono wako ili kuponya wagonjwa na kutenda ishara na miujiza kwa jina la Mwanao mtakatifu Isa.”
31Walipokwisha kuomba, mahali walipokuwa wamekutanika pakatikiswa, wote wakajazwa na Roho Mtakatifu wa Mungu, wakanena neno la Mungu kwa ujasiri.
Waumini washirikiana mali yao
32Waumini wote walikuwa na moyo mmoja na nia moja. Wala hakuna hata mmoja aliyesema chochote alichokuwa nacho ni mali yake mwenyewe, lakini walishirikiana kila kitu walichokuwa nacho. 33Mitume wakatoa ushuhuda wa kufufuka kwa Bwana Isa kwa nguvu nyingi na neema ya Mungu ilikuwa juu yao wote. 34Wala hapakuwa mtu yeyote miongoni mwao aliyekuwa mhitaji, kwa sababu mara kwa mara wale waliokuwa na mashamba na nyumba waliviuza, wakaleta thamani ya vitu vilivyouzwa, 35wakaiweka miguuni pa mitume, kila mtu akagawiwa kadiri ya mahitaji yake.
36Yusufu, Mlawi kutoka Kipro, ambaye mitume walimwita Barnaba (maana yake Mwana wa Faraja), 37aliuza shamba alilokuwa nalo, akaleta hizo fedha alizopata na kuziweka miguuni pa mitume.
Iliyochaguliwa sasa
Matendo 4: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapi.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.