Matendo 28
28
Paulo kisiwani Malta
1Baada ya kufika nchi kavu salama, ndipo tukafahamu kwamba jina la kile kisiwa ni Malta. 2Wenyeji wa kile kisiwa walituonesha ukarimu usio wa kawaida. Waliwasha moto na kutukaribisha sisi sote kwa sababu mvua ilikuwa inanyesha na kulikuwa na baridi. 3Paulo alikusanya mzigo wa kuni, na alipokuwa anaweka kuni kwenye moto, nyoka mwenye sumu akatoka humo kwa ajili ya joto na kujisokotea mkononi mwake. 4Wale wenyeji wa kile kisiwa walipomwona yule nyoka akining’inia mkononi mwa Paulo, wakaambiana, “Huyu mtu lazima awe ni muuaji, ingawa ameokoka kutoka baharini, haki haijamwacha aishi.” 5Lakini Paulo akamkung’utia yule nyoka ndani ya moto wala yeye hakupata madhara yoyote. 6Watu walikuwa wanangoja avimbe au aanguke ghafula na kufa. Lakini baada ya kungoja kwa muda mrefu na kuona kwamba hakuna chochote kisicho cha kawaida kilichomtokea, wakabadili mawazo yao na kuanza kusema kwamba yeye ni mungu.
7Basi karibu na sehemu ile, palikuwa na shamba kubwa la kiongozi mkuu wa kile kisiwa, aliyeitwa Publio. Alitupokea kwake, na akatuhudumia kwa ukarimu mkubwa kwa muda wa siku tatu. 8Baba yake Publio alikuwa mgonjwa kitandani, akiwa anaugua homa na kuhara damu. Paulo akaingia ndani ili kumwona na baada ya maombi, akaweka mikono juu yake na kumponya. 9Jambo hili lilipotukia, watu wote wa kisiwa kile waliokuwa wagonjwa wakaja, nao wakaponywa. 10Wakatupatia heshima nyingi, nasi tulipokuwa tayari kusafiri kwa meli, wakatupakilia vitu vyote tulivyokuwa tunavihitaji.
Paulo awasili Rumi
11Miezi mitatu baadaye tukaanza safari kwa meli iliyokuwa imetia nanga kwenye kisiwa hicho kwa ajili ya majira ya baridi. Hii ilikuwa meli ya Iskanderia yenye alama ya miungu pacha waitwao Kasta na Poluksi. 12Kituo chetu cha kwanza kilikuwa Sirakusa na tukakaa huko siku tatu. 13Kisha tukang’oa nanga, tukafika Regio. Siku iliyofuata, upepo mkali wa kusi ukavuma, na siku ya pili yake tukafika Puteoli. 14Huko tukawakuta ndugu, nasi tukakaribishwa tukae nao kwa siku saba. Hivyo tukaendelea na safari hadi Rumi. 15Ndugu wa huko Rumi waliposikia habari zetu, walikuja hadi Soko la Apio na mahali paitwapo Mikahawa Mitatu kutulaki. Paulo alipowaona, alimshukuru Mungu akatiwa moyo. 16Tulipofika Rumi, Paulo aliruhusiwa kuishi peke yake akiwa na askari wa kumlinda.
Paulo ahubiri Rumi chini ya ulinzi
17Siku tatu baadaye Paulo akawaita pamoja viongozi wa Wayahudi. Walipokwisha kukusanyika akawaambia, “Ndugu zangu, ingawa sikufanya jambo lolote dhidi ya watu wetu au dhidi ya desturi za baba zetu, lakini nilikamatwa huko Yerusalemu nikakabidhiwa kwa Warumi. 18Wao walipokwisha kunihoji, wakataka kuniachia huru kwa sababu hawakuona kosa lolote nililolifanya linalostahili adhabu ya kifo. 19Lakini Wayahudi walipopinga uamuzi huo, nililazimika kukata rufaa kwa Kaisari, ingawa sikuwa na lalamiko lolote juu ya taifa langu. 20Basi hii ndiyo sababu nimewatumania, ili niseme nanyi. Kwa kuwa ni kwa ajili ya tumaini la Israeli nimefungwa kwa minyororo.”
21Wakamjibu, “Hatujapokea barua zozote kutoka Yudea zinazokuhusu, wala hapana ndugu yeyote aliyekuja hapa ambaye ametoa taarifa au kuzungumza jambo lolote baya juu yako. 22Lakini tungependa kusikia kutoka kwako unalofikiri kwa sababu tunajua kwamba kila mahali watu wanazungumza mabaya kuhusu jamii hii.”
23Baada ya kupanga siku ya kuonana naye, watu wengi wakaja kuanzia asubuhi hadi jioni akawaeleza na kutangaza kuhusu ufalme wa Mungu akijaribu kuwahadithia juu ya Isa kutoka Torati ya Musa na kutoka Manabii. 24Baadhi wakasadiki yale aliyosema, lakini wengine hawakuamini. 25Hivyo hawakukubaliana, nao walipokuwa wanaondoka, Paulo akatoa kauli moja zaidi: “Roho wa Mungu alinena kweli na baba zenu aliposema mambo yale yaliyomhusu Bwana Isa kwa kinywa cha nabii Isaya kwamba:
26“ ‘Nenda kwa watu hawa na useme,
“Hakika mtasikiliza lakini hamtaelewa;
na pia mtatazama, lakini hamtaona.”
27Kwa kuwa mioyo ya watu hawa imekuwa migumu;
hawasikii kwa masikio yao,
na wamefumba macho yao.
Wasije wakaona kwa macho yao,
na wakasikiliza kwa masikio yao,
wakaelewa kwa mioyo yao,
na kugeuka nami nikawaponya.’#28:27 Isaya 6:9, 10
28“Basi na ijulikane kwenu kwamba, huu wokovu wa Mungu umepelekwa kwa watu wa Mataifa, nao watasikiliza.” [ 29Baada yake kusema maneno haya, Wayahudi wakaondoka wakiwa na hoja nyingi miongoni mwao.]#28:29 Maandiko mengine ya kale hayana maneno haya.
30Kwa miaka miwili mizima Paulo alikaa huko kwa nyumba aliyokuwa amepanga. Akawakaribisha wote walioenda kumwona. 31Akahubiri ufalme wa Mungu na kufundisha mambo yale yaliyomhusu Bwana Isa Al-Masihi, kwa ujasiri wote na bila kizuizi chochote.
Iliyochaguliwa sasa
Matendo 28: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.