Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 27:27-44

Matendo 27:27-44 NENO

Usiku wa kumi na nne ulipofika, tulikuwa bado tunasukumwa na upepo katika Bahari ya Adria. Ilipokuwa yapata usiku wa manane, mabaharia wakahisi kwamba walikuwa wanakaribia nchi kavu. Kwa hiyo wakapima kina cha maji na kukuta kilikuwa pima ishirini; baada ya kuendelea mbele kidogo, wakapima tena wakapata kina cha pima kumi na tano. Wakiogopa kwamba meli yetu ingegonga kwenye miamba, wakashusha nanga nne za nyuma ya meli, wakawa wanaomba kupambazuke. Katika jaribio la kutoroka kutoka kwa meli, mabaharia wakashusha mashua ya kuokolea watu baharini, wakijifanya kwamba wanaenda kushusha nanga za omo. Ndipo Paulo akamwambia yule jemadari na askari, “Hawa watu wasipobaki katika meli, hamtaweza kuokoka.” Hivyo basi wale askari wakakata kamba zilizoshikilia ile mashua ya kuokolea watu kwenye meli, wakaiacha ianguke humo baharini. Kabla ya mapambazuko, Paulo akawasihi watu wote wale chakula akisema, “Leo ni siku ya kumi na nne mmekuwa katika wasiwasi mkiwa mmefunga na bila kula chochote. Kwa hiyo nawasihi mle chakula, kwa maana itawasaidia ili mweze kuishi. Kwa kuwa hakuna hata mmoja wenu atakayepoteza unywele hata mmoja kutoka kichwani mwake.” Baada ya kusema maneno haya, Paulo akachukua mkate, akamshukuru Mungu mbele yao wote, akaumega akaanza kula. Ndipo wote wakatiwa moyo, wakaanza kula chakula. Ndani ya meli tulikuwa jumla ya watu mia mbili na sabini na sita (276). Baada ya watu wote kula chakula cha kutosha, wakapunguza uzito wa meli kwa kutupa ngano baharini. Kulipopambazuka, mabaharia hawakuitambua ile nchi, lakini waliona ghuba yenye ufuko wa mchanga, ambako waliamua kuipweleza meli kama ingewezekana. Kwa hiyo wakatupa nanga zote na kuziacha baharini, na wakati huo huo wakalegeza kamba zilizokuwa zikishikilia usukani wa meli. Kisha wakatweka tanga la mbele lishike upepo na kuisukuma meli kuelekea pwani. Lakini wakafika mahali bahari mbili zinakutana, wakaipweleza meli ufuoni; omo ikakwama sana, ikawa haiwezi kuondolewa; lakini sehemu ya shetri ikavunjika vipande vipande kutokana na kupigwa kwa mawimbi yenye nguvu. Wale askari wakapanga kuwaua wale wafungwa ili kuzuia hata mmoja wao asiogelee na kutoroka. Lakini yule jemadari alitaka kuokoa maisha ya Paulo, basi akawazuia askari wasitekeleze mpango wao. Akaamuru wale wanaoweza kuogelea wajitupe baharini kwanza, waogelee hadi nchi kavu. Waliosalia wangefika nchi kavu kwa kutumia mbao au vipande vya meli iliyovunjika, hivyo wote wakafika nchi kavu salama.

Video ya Matendo 27:27-44