Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 21:17-26

Matendo 21:17-26 NENO

Tulipofika Yerusalemu, ndugu wakatukaribisha kwa furaha. Kesho yake Paulo pamoja na wengine wetu tulienda kumwona Yakobo, na wazee wote walikuwako. Baada ya kuwasalimu, Paulo akatoa taarifa kamili ya mambo yote ambayo Mungu alikuwa amefanya miongoni mwa watu wa Mataifa kupitia huduma yake. Baada ya kusikia mambo haya, wakamsifu Mungu. Ndipo wakamwambia Paulo, “Ndugu, unaona kulivyo na maelfu ya Wayahudi walioamini, nao wote wana juhudi kwa ajili ya sheria. Lakini wameambiwa habari zako kwamba unafundisha Wayahudi wote wanaoishi miongoni mwa watu wa Mataifa kumkataa Musa, na kwamba unawaambia wasiwatahiri watoto wao wala kufuata desturi zetu. Sasa tufanyeje? Bila shaka watasikia kwamba umekuja Yerusalemu. Kwa hiyo fanya lile tunalokuambia. Tuna watu wanne hapa ambao wameweka nadhiri. Jiunge na watu hawa, mfanye utaratibu wa ibada ya kujitakasa pamoja nao, na ulipe gharama ili wanyoe nywele zao. Kwa njia hii kila mtu atafahamu ya kuwa mambo waliyosikia si ya kweli na kwamba wewe unaishika sheria. Lakini kuhusu wale watu wa Mataifa walioamini, tumewaandikia uamuzi wetu: kwamba wajitenge na vyakula vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na damu, au kula nyama ya mnyama aliyenyongwa, na wajiepushe na uasherati.” Ndipo kesho yake Paulo akaenda na wale watu, akajitakasa pamoja nao. Akaingia ndani ya Hekalu ili atoe taarifa ya tarehe ambayo siku zao za utakaso zingemalizika na sadaka ingetolewa kwa ajili ya kila mmoja wao.

Video ya Matendo 21:17-26