Matendo 2:1-13
Matendo 2:1-13 NEN
Siku ya Pentekoste ilipowadia, waamini wote walikuwa mahali pamoja. Ghafula sauti kama mvumo mkubwa wa upepo mkali uliotoka mbinguni ukaijaza nyumba yote walimokuwa wameketi. Zikatokea ndimi kama za moto zilizogawanyika na kukaa juu ya kila mmoja wao. Wote wakajazwa na Roho Mtakatifu, wakaanza kunena kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia. Basi walikuwepo Yerusalemu Wayahudi wanaomcha Mungu kutoka kila taifa chini ya mbingu. Waliposikia sauti hii, umati wa watu ulikusanyika pamoja wakistaajabu, kwa sababu kila mmoja wao aliwasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe. Wakiwa wameshangaa na kustaajabu wakauliza, “Je, hawa wote wanaozungumza si Wagalilaya? Imekuwaje basi kila mmoja wetu anawasikia wakinena kwa lugha yake ya kuzaliwa? Wapathi, Wamedi, Waelami, wakazi wa Mesopotamia, Uyahudi, Kapadokia, Ponto na Asia, Frigia, Pamfilia, Misri na pande za Libya karibu na Kirene na wageni kutoka Rumi, Wayahudi na waongofu, Wakrete na Waarabu, sote tunawasikia watu hawa wakisema mambo makuu ya ajabu ya Mungu katika lugha zetu wenyewe.” Wakiwa wameshangaa na kufadhaika wakaulizana, “Ni nini maana ya mambo haya?” Lakini wengine wakawadhihaki wakasema, “Hawa wamelewa divai!”