2 Timotheo 2:1-13
2 Timotheo 2:1-13 NEN
Basi, wewe mwanangu, uwe hodari katika neema iliyo ndani ya Kristo Yesu. Nayo mambo yale uliyonisikia nikiyasema mbele ya mashahidi wengi, uwakabidhi watu waaminifu watakaoweza kuwafundisha watu wengine vilevile. Vumilia taabu pamoja nasi kama askari mwema wa Kristo Yesu. Hakuna askari yeyote ambaye akiwa vitani hujishughulisha na mambo ya kawaida ya maisha haya kwa sababu nia yake ni kumpendeza yule aliyemwandika awe askari. Vivyo hivyo, yeye ashindanaye katika michezo hawezi kupewa tuzo ya ushindi asiposhindana kulingana na kanuni za mashindano. Mkulima mwenye bidii ya kazi ndiye anayestahili kuwa wa kwanza kupata fungu la mavuno. Fikiri sana kuhusu haya nisemayo, kwa maana Bwana atakupa ufahamu katika mambo hayo yote. Mkumbuke Yesu Kristo, aliyefufuliwa kutoka kwa wafu, yeye aliye wa uzao wa Daudi. Hii ndiyo Injili yangu, ambayo kwayo ninateseka hata kufikia hatua ya kufungwa minyororo kama mhalifu. Lakini neno la Mungu halifungwi. Kwa hiyo ninavumilia mambo yote kwa ajili ya wateule wa Mungu, kusudi wao nao wapate wokovu ulio katika Kristo Yesu, pamoja na utukufu wa milele. Hili ni neno la kuaminiwa: Kwa maana kama tumekufa pamoja naye, tutaishi pia pamoja naye. Kama tukistahimili, pia tutatawala pamoja naye. Kama tukimkana yeye, naye atatukana sisi. Kama tusipoamini, yeye hudumu kuwa mwaminifu, kwa maana hawezi kujikana mwenyewe.