2 Timotheo 1
1
Salamu
1Paulo mtume wa Al-Masihi Isa kwa mapenzi ya Mungu, kulingana na ile ahadi ya uzima ulio ndani ya Al-Masihi Isa.
2Kwa Timotheo, mwanangu mpendwa.
Neema, rehema na amani zinazotoka kwa Mungu Baba#1:2 Kwa mwanadamu, Mwenyezi Mungu ni Baba kupitia uhusiano unaopatikana katika kumtumaini Isa Al-Masihi. Mwenyezi, na kwa Al-Masihi Isa, Bwana wetu.
Shukrani na kutiwa moyo
3Ninamshukuru Mungu, ninayemtumikia kwa dhamiri safi kama walivyofanya baba zangu, ninapokukumbuka usiku na mchana katika maombi yangu. 4Nikiyakumbuka machozi yako, ninatamani sana kukuona ili nipate kujawa na furaha. 5Nimekuwa nikiikumbuka imani yako ya kweli, waliokuwa nayo bibi yako Loisi na mama yako Eunike, na ninasadiki sasa wewe pia unayo.
6Kwa sababu hii nakukumbusha uchochee ile karama ya Mungu iliyowekwa ndani yako nilipokuwekea mikono yangu. 7Maana Mungu hakutupatia roho ya woga, bali roho ya nguvu, ya upendo na ya moyo wa kiasi.
8Kwa hiyo usione haya kushuhudia kuhusu Bwana wetu, wala usinionee haya mimi niliye mfungwa kwa ajili yake. Bali uishiriki pamoja nami taabu ya Injili, kwa kadiri ya nguvu ya Mungu, 9ambaye alituokoa na kutuita katika mwito mtakatifu: si kwa kadiri ya matendo yetu mema, bali kwa sababu ya kusudi lake mwenyewe na neema yake. Neema hii tulipewa katika Al-Masihi Isa tangu milele. 10Lakini sasa imefunuliwa kwa kudhihirishwa kwake Mwokozi wetu, Al-Masihi Isa, ambaye amebatilisha mauti na kuleta uzima na kutokufa kupitia kwa Injili. 11Nami nimewekwa kuwa mhubiri, mtume na mwalimu wa Injili hii. 12Hii ndiyo sababu ninateseka namna hii, lakini sioni haya kwa maana ninamjua yeye niliyemwamini, na kusadiki ya kuwa anaweza kukilinda kile nilichokiweka amana kwake hadi siku ile.
13Shika kwa uthabiti kielelezo cha mafundisho yenye uzima uliyoyasikia kwangu, pamoja na imani na upendo katika Al-Masihi Isa. 14Ilinde ile amana uliyokabidhiwa kwa Roho wa Mungu akaaye ndani yetu.
15Unajua ya kuwa watu wote katika jimbo la Asia wameniacha, miongoni mwao wamo Filego na Hermogene.
16Bwana Isa akawahurumie watu wa nyumbani mwa Onesiforo, kwa sababu aliniburudisha mara kwa mara, wala hakuionea aibu minyororo yangu. 17Badala yake, alipokuwa Rumi alinitafuta kwa bidii hadi akanipata. 18Bwana Isa na amjalie kupata rehema zake siku ile! Nawe unajua vyema jinsi alivyonisaidia huko Efeso.
Iliyochaguliwa sasa
2 Timotheo 1: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapi.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.