2 Samweli 5:1-16
2 Samweli 5:1-16 NENO
Makabila yote ya Israeli yakamjia Daudi huko Hebroni na kumwambia, “Sisi tu mwili wako na damu yako. Zamani, wakati Sauli alikuwa mfalme juu yetu, wewe ndiwe uliyeiongoza Israeli vitani. Naye Mwenyezi Mungu alikuambia, ‘Wewe utawachunga watu wangu Israeli, na utakuwa mtawala wao.’ ” Wazee wote wa Israeli wakamwendea Mfalme Daudi huko Hebroni, mfalme akafanya mapatano nao huko Hebroni mbele za Mwenyezi Mungu, nao wakampaka Daudi mafuta kuwa mfalme wa Israeli. Daudi alikuwa na umri wa miaka thelathini alipoanza kutawala, naye akatawala Israeli kwa miaka arobaini. Huko Hebroni alitawala Yuda kwa miaka saba na miezi sita, na katika Yerusalemu alitawala Israeli yote na Yuda kwa miaka thelathini na tatu. Mfalme na watu wake wakaenda Yerusalemu kuwashambulia Wayebusi walioishi humo. Wayebusi wakamwambia Daudi, “Wewe hutaingia humu, kwani hata vipofu na viwete wanaweza kukufukuza.” Walidhani, “Daudi hawezi kuingia humu.” Hata hivyo, Daudi akaiteka ngome ya Sayuni, Mji wa Daudi. Siku ile, Daudi akasema, “Yeyote ambaye atawashinda Wayebusi, atatumia huo mfereji kuwafikia hao ‘viwete na vipofu’ ambao ni adui za Daudi.” Ndiyo sababu wanasema, “ ‘Vipofu na viwete’ hawataingia kwenye jumba la ufalme.” Ndipo Daudi akafanya makao ndani ya ngome na kuiita Mji wa Daudi. Akajenga eneo linalozunguka kuanzia Milo kuelekea ndani. Daudi akazidi kuwa na nguvu zaidi na zaidi, kwa sababu Bwana Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, alikuwa pamoja naye. Basi Hiramu mfalme wa Tiro akawatuma wajumbe kwa Daudi, wakiwa na magogo ya mwerezi, maseremala na waashi, nao wakajenga jumba la kifalme kwa ajili ya Daudi. Naye Daudi akafahamu kuwa Mwenyezi Mungu amemwimarisha kuwa mfalme juu ya Israeli na ameinua ufalme wake kwa ajili ya Israeli, watu wake. Baada ya Daudi kuondoka Hebroni, akajitwalia masuria zaidi na wake huko Yerusalemu, nao wana wengi wa kiume na wa kike walizaliwa kwake. Haya ndiyo majina ya watoto waliozaliwa kwake huko: Shamua, Shobabu, Nathani, Sulemani, Ibihari, Elishua, Nefegi, Yafia, Elishama, Eliada na Elifeleti.