2 Samweli 21:15-22
2 Samweli 21:15-22 NEN
Kwa mara nyingine tena kulikuwa na vita kati ya Wafilisti na Israeli. Daudi akashuka pamoja na watu wake ili kupigana dhidi ya Wafilisti, naye akawa amechoka sana. Naye Ishbi-Benobu, mmoja wa wazao wa Warefai, ambaye mkuki wake ulikuwa na uzito wa shekeli 300 za shaba, alikuwa amejifunga upanga mpya, naye alisema angemuua Daudi. Lakini Abishai mwana wa Seruya akaja kumwokoa Daudi; akampiga huyo Mfilisti, akamwangusha chini na kumuua. Ndipo watu wakamwapia Daudi, wakisema, “Kamwe hutakwenda tena nasi vitani, ili kwamba taa ya Israeli isije ikazimwa.” Baada ya muda, kukawa na vita nyingine na Wafilisti, huko Gobu. Wakati huo Sibekai, Mhushathi, akamuua Safu, mmoja wa wazao wa Warefai. Katika vita vingine na Wafilisti huko Gobu, Elhanani mwana wa Yaare-Oregimu, Mbethlehemu, alimuua nduguye Goliathi, Mgiti, ambaye mkuki wake ulikuwa na mpini kama mti wa mfumaji. Katika vita vingine tena, vilivyopiganwa huko Gathi, kulikuwako na mtu mmoja mkubwa mwenye vidole sita katika kila mkono na vidole sita kila mguu, jumla vidole ishirini na vinne. Yeye alikuwa pia mzao wa Mrefai. Alipowadhihaki Israeli, Yonathani mwana wa Shimea, nduguye Daudi, akamuua. Hawa wanne walikuwa wazao wa Warefai huko Gathi, nao walianguka kwa mikono ya Daudi na watu wake.