Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Samweli 21:1-14

2 Samweli 21:1-14 NEN

Wakati wa utawala wa Daudi kulikuwa na njaa kwa miaka mitatu mfululizo, kwa hiyo Daudi akautafuta uso wa BWANA. BWANA akasema, “Ni kwa sababu ya Sauli na nyumba yake iliyotiwa madoa ya damu, kwa sababu aliwaua Wagibeoni.” Mfalme akawaita Wagibeoni na kuzumgumza nao. (Wagibeoni hawakuwa wa wana wa Israeli, ila walikuwa mabaki ya Waamori. Waisraeli walikuwa wameapa kuwaacha hai, lakini Sauli katika wivu wake kwa ajili ya Israeli na Yuda, alikuwa amejaribu kuwaangamiza.) Daudi akawauliza Wagibeoni, “Niwatendee nini? Nitawaridhishaje ili mbariki urithi wa BWANA?” Wagibeoni wakamjibu, “Hatuna haki ya kudai fedha wala dhahabu kutoka kwa Sauli au jamaa yake, wala hatuna haki ya kumuua mtu yeyote katika Israeli.” Daudi akawauliza, “Mnataka niwafanyie nini?” Wakamjibu mfalme, “Kwa habari ya mtu aliyetuangamiza na kufanya hila mbaya dhidi yetu ili kwamba tuangamizwe na tusiwe na yeyote katika Israeli, tupatieni wazao wake saba wa kiume tuwaue hadharani mbele za BWANA huko Gibea ya Sauli, aliyekuwa amechaguliwa na BWANA.” Basi mfalme akasema, “Nitawakabidhi kwenu.” Mfalme akamhifadhi Mefiboshethi mwana wa Yonathani, mwana wa Sauli, kwa sababu ya kile kiapo mbele za BWANA kati ya Daudi na Yonathani. Lakini mfalme akamchukua Armoni na Mefiboshethi, wana wawili wa Rispa binti Aiya, ambao alikuwa amemzalia Sauli, pamoja na wana watano wa Merabu binti Sauli, aliokuwa amemzalia Adrieli mwana wa Barzilai, Mmeholathi. Akawakabidhi kwa Wagibeoni, ambao waliwaua na kuwaweka wazi juu ya kilima mbele za BWANA. Wote saba walianguka kwa pamoja; waliuawa katika siku za kwanza za mavuno, mara tu uvunaji wa shayiri ulipokuwa unaanza. Rispa binti Aiya akachukua nguo ya gunia, akajitandikia juu ya mwamba. Kuanzia mwanzo wa mavuno mpaka mvua ziliponyesha juu ya miili ya hao waliouawa, Rispa hakuruhusu ndege wa angani kuwagusa wakati wa mchana, wala wanyama wa mwitu wakati wa usiku. Daudi alipoambiwa kile Rispa binti Aiya, suria wa Sauli, alichokuwa amekifanya, alikwenda akachukua mifupa ya Sauli na mwanawe Yonathani kutoka kwa watu wa Yabeshi-Gileadi. (Walikuwa wameichukua kwa siri kutoka uwanja wa watu wote huko Beth-Shani, mahali ambapo Wafilisti walikuwa wamewatundika baada ya kumuua Sauli huko Gilboa.) Daudi akaileta mifupa ya Sauli na ya mwanawe Yonathani kutoka huko, pia mifupa ya wale waliokuwa wameuawa na kutupwa ilikusanywa. Wakazika mifupa ya Sauli na ya mwanawe Yonathani katika kaburi la Kishi, babaye Sauli, huko Sela katika nchi ya Benyamini, nao wakafanya kila kitu mfalme alichoagiza. Baada ya hayo, Mungu akajibu maombi kwa ajili ya nchi.