Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Samweli 19:11-23

2 Samweli 19:11-23 NENO

Mfalme Daudi akapeleka ujumbe huu kwa makuhani Sadoki na Abiathari, kusema: “Waulizeni wazee wa Yuda, ‘Kwa nini mwe wa mwisho kumrudisha mfalme katika jumba lake la kifalme, maadamu kile kinachosemwa katika Israeli yote kimemfikia mfalme katika makao yake? Ninyi ni ndugu zangu, mwili wangu na damu yangu mwenyewe. Kwa hiyo kwa nini mwe wa mwisho kumrudisha mfalme?’ Nanyi mwambieni Amasa, ‘Je, wewe si mwili wangu mwenyewe na damu yangu? Mungu na aniadhibu vikali zaidi, kama kuanzia sasa na kuendelea wewe si jemadari wa jeshi langu mahali pa Yoabu.’ ” Alivutia mioyo ya watu wote wa Yuda, kama vile walikuwa mtu mmoja. Wakapeleka ujumbe kwa mfalme, kusema, “Rudi, wewe na watumishi wako wote.” Ndipo mfalme akarudi, akaenda hadi kufikia Mto Yordani. Basi watu wa Yuda walikuwa wamekuja Gilgali ili kutoka kwenda kumlaki mfalme na kumvusha Mto Yordani. Shimei mwana wa Gera, wa kabila la Benyamini kutoka Bahurimu, akaharakisha kuteremka pamoja na wanaume wa Yuda ili kumlaki Mfalme Daudi. Pamoja naye walikuwa Wabenyamini elfu moja wakiwa wamefuatana na Siba, msimamizi wa nyumba ya Sauli, pia wanawe kumi na watano, na watumishi ishirini. Wakaharakisha kwenda Yordani, mahali mfalme alipokuwa. Wakavuka kivuko ili kuwachukua watu wa nyumbani mwa mfalme ili kuwavusha na kufanya kila kitu alichotaka. Shimei mwana wa Gera alipovuka Yordani, akaanguka kifudifudi mbele ya mfalme, na kumwambia, “Bwana wangu na asinihesabie hatia. Usikumbuke jinsi mtumishi wako alivyofanya kosa siku ile bwana wangu mfalme alipoondoka Yerusalemu. Mfalme aliondoe moyoni mwake. Kwa maana mimi mtumishi wako najua nimefanya dhambi, lakini leo nimekuja hapa kama wa kwanza wa nyumba yote ya Yusufu kushuka na kumlaki bwana wangu mfalme.” Ndipo Abishai mwana wa Seruya akasema, “Je, Shimei hapaswi kuuawa kwa ajili ya hili? Alimlaani mpakwa mafuta wa Mwenyezi Mungu.” Daudi akajibu, “Mimi nina nini nanyi, enyi wana wa Seruya? Siku ya leo mmekuwa adui zangu! Je, leo kuna yeyote atakayeuawa katika Israeli? Je, mimi sijui kuwa leo ndimi mfalme katika Israeli yote?” Basi mfalme akamwambia Shimei, “Hutakufa.” Naye mfalme akamwahidi kwa kiapo.