Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Samweli 19:1-10

2 Samweli 19:1-10 NEN

Yoabu akaambiwa, “Mfalme analia na kumwombolezea Absalomu.” Kwa jeshi lote, ushindi wa siku ile ukageuka kuwa maombolezo, kwa sababu siku ile vikosi vilisikia ikisemwa, “Mfalme anahuzunika kwa ajili ya mwanawe.” Siku ile watu wakaingia mjini kimya kama vile waingiavyo kwa aibu watu waliokimbia kutoka vitani. Mfalme akafunika uso wake akalia kwa sauti, akisema, “Ee mwanangu Absalomu! Ee Absalomu, mwanangu, mwanangu!” Kisha Yoabu akaingia ndani ya nyumba ya mfalme na kusema, “Leo umewaaibisha watu wako wote, waliookoa maisha yako, maisha ya wanao na binti zako, maisha ya wake zako na masuria wako. Unawapenda wale wanaokuchukia, na unawachukia wale wanaokupenda. Leo umeonyesha wazi kwamba majemadari wako na watu wao hawana maana kwako. Naona kwamba ungefurahi kama Absalomu angekuwa hai leo na sisi sote tuwe tumekufa. Sasa utoke nje ukawatie moyo watu wako. Naapa kwa BWANA kwamba ikiwa hutatoka nje, hakuna mtu atakayesalia pamoja nawe ifikapo leo jioni. Hii itakuwa mbaya zaidi kwako kuliko maafa yote yaliyokupata tangu ujana wako hadi sasa.” Kwa hiyo mfalme akaondoka akaketi kitini pake penye lango. Watu walipoambiwa, “Mfalme ameketi langoni,” watu wote wakamjia. Wakati huo, Waisraeli walikuwa wamekimbilia nyumbani kwao. Katika makabila yote ya Israeli, watu walikuwa wanabishana wao kwa wao, wakisema, “Mfalme alituokoa kutoka mikononi mwa adui zetu; ndiye alituokoa kutoka mikononi mwa Wafilisti. Lakini sasa mfalme ameikimbia nchi kwa sababu ya Absalomu, naye Absalomu, tuliyemtia mafuta atutawale, amekufa vitani. Basi mbona hamsemi lolote kuhusu kumrudisha mfalme?”