2 Samweli 14
14
Absalomu arudi Yerusalemu
1Yoabu mwana wa Seruya akafahamu kuwa moyo wa mfalme ulikuwa na shauku ya kumwona Absalomu. 2Kwa hiyo Yoabu akamtuma mtu kwenda Tekoa na kumleta mwanamke mwenye hekima kutoka huko. Akamwambia huyo mwanamke, “Jifanye uko katika maombolezo. Vaa nguo za kuomboleza, nawe usitumie mafuta yoyote ya urembo. Jifanye kama mwanamke ambaye amekuwa na huzuni kwa siku nyingi kwa ajili ya kufiwa. 3Kisha nenda kwa mfalme ukazungumze maneno haya.” Naye Yoabu akaweka maneno kinywani mwa yule mwanamke.
4Huyo huyo mwanamke kutoka Tekoa alipofika kwa mfalme, akaanguka kifudifudi kumpa mfalme heshima, akasema, “Ee mfalme, nisaidie!”
5Mfalme akamuuliza, “Una shida gani?”
Akamwambia, “Mimi ni mjane, mume wangu amekufa. 6Mimi mtumishi wako nilikuwa na wana wawili. Wakapigana wao kwa wao huko shambani wala huko hapakuwa na mtu hata mmoja wa kuwatenganisha. Mmoja akampiga mwenzake na kumuua. 7Sasa ukoo wote umeinuka dhidi ya mtumishi wako, wakisema, ‘Utukabidhi huyo aliyemuua ndugu yake, ili tumuue kwa ajili ya uhai wa ndugu yake aliyemuua, nasi hapo tutakuwa tumekatilia mbali na mrithi pia.’ Wakifanya hivyo, watakuwa wamezima tumaini langu lililobaki, mume wangu hataachiwa jina wala mzao katika uso wa dunia.”
8Mfalme akamwambia huyo mwanamke, “Nenda nyumbani, nami nitatoa agizo kwa ajili yako.”
9Lakini huyo mwanamke kutoka Tekoa akamwambia, “Mfalme bwana wangu, lawama na iwe juu yangu na juu ya nyumba ya baba yangu, naye mfalme na kiti chake cha utawala asiwe na hatia.”
10Mfalme akajibu, “Ikiwa mtu yeyote atakusemesha lolote, mlete kwangu, naye hatakusumbua tena.”
11Huyo mwanamke akasema, “Basi mfalme na amwombe Mwenyezi Mungu, Mungu wake, ili kuzuia mlipiza kisasi cha damu kuongeza juu ya uharibifu, ili mwanangu asije akaangamizwa.”
Mfalme akasema, “Hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo, hakuna unywele mmoja wa kichwa cha mwanao utakaoanguka chini.”
12Ndipo huyo mwanamke akasema, “Mruhusu mtumishi wako aseme neno kwa mfalme bwana wangu.”
Mfalme akajibu, “Sema.”
13Huyo mwanamke akasema, “Mbona basi wewe umewaza jambo kama hili dhidi ya watu wa Mungu? Je, mfalme asemapo hili, hajitii hatiani mwenyewe, kwa maana mfalme hajamrudisha mwanawe aliyefukuziwa mbali? 14Kama vile maji yaliyomwagika ardhini hayawezi kuzoleka, hivyo sisi kufa ni lazima. Lakini hivyo sivyo Mungu anataka; bali hupanga njia ili mtu aliyefukuzwa asibaki akiwa ametengwa naye.
15“Nami sasa nimekuja kusema hili kwa bwana wangu mfalme kwa sababu watu wameniogopesha. Mtumishi wako alifikiri, ‘Nitanena na mfalme, labda mfalme atamfanyia mtumishi wake kile anachoomba. 16Labda mfalme atakubali kumwokoa mtumishi wake kutoka mkononi mwa mtu anayejaribu kunikatilia mbali, mimi na mwanangu, kutoka urithi Mungu aliotupatia.’
17“Basi sasa mtumishi wako anasema, ‘Neno la bwana wangu mfalme na linipatie pumziko, kwa maana bwana wangu mfalme ni kama malaika wa Mungu katika kutambua jema na baya. Mwenyezi Mungu, Mungu wako, na awe pamoja nawe.’ ”
18Basi mfalme akamwambia huyo mwanamke, “Usinifiche jibu la kile nitakalokuuliza.”
Huyo mwanamke akasema, “Mfalme bwana wangu na aseme.”
19Mfalme akauliza, “Je, mkono wa Yoabu haupo pamoja nawe katika jambo hilo lote?”
Huyo mwanamke akajibu, “Hakika kama uishivyo, bwana wangu mfalme, hakuna yeyote anayeweza kugeuka kulia wala kushoto kutokana na chochote anachosema bwana wangu mfalme. Naam, ni mtumishi wako Yoabu ndiye alinifundisha kufanya hivi, naye ndiye aliweka maneno haya yote kinywani mwa mtumishi wako. 20Mtumishi wako Yoabu amefanya hivi ili kubadili hali iliyopo. Bwana wangu ana hekima kama ile ya malaika wa Mungu, anafahamu kila kitu kinachotokea katika nchi.”
21Mfalme akamwambia Yoabu, “Vyema sana, nitalifanya jambo hili. Nenda, ukamlete kijana Absalomu.”
22Yoabu akasujudu uso wake ukielekea chini ili kumpa mfalme heshima, na akambariki mfalme. Yoabu akasema, “Leo mtumishi wako anajua kuwa amepata kibali machoni pako, bwana wangu mfalme, kwa sababu mfalme amemjalia mtumishi wake ombi lake.”
23Ndipo Yoabu akaenda hadi Geshuri akamrudisha Absalomu Yerusalemu. 24Lakini mfalme akasema, “Lazima Absalomu aende kwenye nyumba yake mwenyewe; kamwe asiuone uso wangu.” Kwa hiyo Absalomu akaenda kwenye nyumba yake na hakuuona uso wa mfalme.
25Katika Israeli yote hakuna mtu yeyote aliyesifiwa kwa uzuri wa sura kama Absalomu. Kuanzia utosi wa kichwa chake hadi wayo wa mguu wake hakuwa na kasoro. 26Kila mara aliponyoa nywele za kichwa chake, kwa kuwa alizinyoa nywele zake mara moja kwa mwaka kwa sababu zilikuwa nzito sana kwake, alizipima; uzito wake ulikuwa shekeli mia mbili kwa kipimo cha kifalme#14:26 Shekeli 200 kwa kipimo cha kifalme ni sawa na kilo 2.3..
27Walizaliwa wana watatu na binti mmoja kwa Absalomu. Jina la binti yake aliitwa Tamari, naye akawa mwanamke mzuri wa sura.
28Absalomu akaishi miaka miwili huko Yerusalemu pasipo kuuona uso wa mfalme. 29Basi Absalomu akamtumania Yoabu kwa kusudi la kumtuma kwa mfalme, lakini Yoabu akakataa kuja kwa Absalomu. Ndipo akamtumania mara ya pili, lakini pia akakataa kuja. 30Ndipo akawaambia watumishi wake, “Tazama, shamba la Yoabu liko jirani na langu, naye ana shayiri humo. Nendeni mkaitie moto.” Kisha watumishi wa Absalomu wakalitia moto shamba hilo.
31Basi Yoabu akaenda nyumbani mwa Absalomu, akamwambia, “Kwa nini watumishi wako wametia moto shamba langu?”
32Absalomu akamwambia Yoabu, “Tazama, nilikutumia ujumbe na kusema, ‘Njoo ili niweze kukutuma kwa mfalme kuuliza, “Kwa nini nimekuja kutoka Geshuri? Ingekuwa bora zaidi kwangu kama ningebaki huko!” ’ Sasa basi, nataka kuuona uso wa mfalme, na ikiwa nina hatia ya jambo lolote, basi na aniue.”
33Basi Yoabu akaenda kwa mfalme na kumwambia jambo hili. Kisha mfalme akamwita Absalomu, naye akaingia ndani, akasujudu, uso wake ukigusa chini mbele ya mfalme. Naye mfalme akambusu Absalomu.
Iliyochaguliwa sasa
2 Samweli 14: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.