2 Samweli 13:15-22
2 Samweli 13:15-22 NENO
Kisha Amnoni akamchukia Tamari, kwa machukio makuu sana. Kwa kweli, Amnoni alimchukia kuliko alivyokuwa amempenda. Amnoni akamwambia, “Inuka na utoke nje!” Tamari akamwambia, “Hapana! Kunifukuza itakuwa vibaya kuliko yale uliyonitendea.” Lakini Amnoni akakataa kumsikiliza. Akamwita mtumishi wake mahsusi na kumwambia, “Mtoe huyu mwanamke hapa na ufunge mlango nyuma yake.” Kwa hiyo, mtumishi wake akamtoa nje na kufunga mlango nyuma yake. Tamari alikuwa amevaa joho lililopambwa vizuri, kwa maana lilikuwa aina ya mavazi yaliyovaliwa na binti za mfalme waliokuwa mabikira. Tamari akajitia majivu kichwani mwake na kurarua lile joho alilokuwa amevaa. Akaweka mkono wake kichwani, akaenda zake akilia kwa sauti. Absalomu nduguye akamuuliza, “Je, huyo Amnoni ndugu yako, amekutana nawe kimwili? Sasa nyamaza dada yangu; yeye ni ndugu yako. Usilitie jambo hili moyoni.” Naye Tamari akaishi nyumbani mwa Absalomu nduguye, akiwa mwanamke mwenye huzuni. Mfalme Daudi aliposikia mambo haya yote, akakasirika sana. Absalomu hakusema neno lolote, zuri au baya, kwa Amnoni; alimchukia Amnoni kwa sababu alikuwa amemtia aibu Tamari, dada yake.