Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Wafalme 7:1-11

2 Wafalme 7:1-11 NEN

Elisha akasema, “Sikiliza neno la BWANA. Hivi ndivyo asemavyo BWANA: Wakati kama huu kesho, kipimo kimoja cha unga mzuri kitauzwa kwa shekeli moja ya fedha, na vibaba viwili vya shayiri kwa shekeli moja ya fedha katika lango la Samaria.” Yule afisa ambaye mfalme alikuwa anauegemea mkono wake akamwambia yule mtu wa Mungu, “Tazama, hata kama BWANA atafungua madirisha ya mbinguni, je, jambo hili litawezekana?” Elisha akajibu, “Utaona kwa macho yako mwenyewe, lakini wewe hutakula chochote kati ya hivyo!” Basi kulikuwepo na watu wanne wenye ukoma katika ingilio la lango la mji. Wakaambiana, “Kwa nini tukae hapa mpaka tufe? Kama tukisema, ‘Tutaingia mjini,’ mjini kuna njaa, nasi tutakufa humo. Kama tukikaa hapa, tutakufa. Kwa hiyo twende kwenye kambi ya Waaramu na tujisalimishe. Kama wakituacha hai, tutaishi; kama wakituua, basi na tufe.” Wakati wa giza la jioni, wakaondoka na kwenda kwenye kambi ya Waaramu. Walipofika mwanzo wa kambi, hapakuwa na mtu, kwa kuwa Bwana alilifanya jeshi la Waaramu lisikie sauti kama ya magari ya vita, farasi na jeshi kubwa, kiasi kwamba waliambiana, “Tazama, mfalme wa Israeli ameajiri mfalme wa Wahiti na mfalme wa Wamisri kuja kutushambulia sisi!” Kwa hiyo wakaondoka na kukimbia wakati wa giza la jioni na kuacha mahema yao, farasi wao na punda wao. Wakakimbia kuokoa maisha yao na kuacha kila kitu ndani ya kambi kama kilivyokuwa. Wale watu wenye ukoma walipofika mwanzoni mwa kambi, wakaingia kwenye mojawapo ya mahema. Wakala na kunywa, na kuchukua fedha, dhahabu na nguo, wakaenda kuvificha. Wakarudi na kuingia katika hema jingine, na kuchukua baadhi ya vitu kutoka ndani yake na kuvificha pia. Kisha wakaambiana, “Hili tunalolifanya sio jema. Hii ni siku ya habari njema, nasi tunakaa kimya. Kama tukisubiri mpaka mapambazuko, maafa yatatupata. Twendeni mara moja tukatoe habari hizi katika jumba la mfalme.” Hivyo wakaenda mjini na kuwaita walinzi wa langoni, wakawaambia, “Tulikwenda katika kambi ya Waaramu lakini hapakuwepo na mtu huko, hata sauti ya mtu yeyote, ila farasi na punda waliofungwa na mahema yaliyoachwa kama yalivyokuwa.” Walinzi wa langoni wakatangaza habari ile kwa sauti kuu, na taarifa hii ikatolewa ndani ya jumba la mfalme.